Mkurugenzi
wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii (SSRA), Bw. Onorius Njole akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mpango Maalum wa kutoa huduma ya hifadhi
ya jamii kwa sekta isiyo rasmi maarufu kama Informal Sector Scheme
ambayo inajumuisha waendesha bodaboda, bajaji na mama lishe. Kulia ni
Mkuu wa Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Bi. Sarah Kibonde.
Mkuu
wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji kutoka Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bi. Sarah Kibonde
akiwaeleza waandishi wa habari juhudi za Serikali katika kuboresha na
kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya jamii hasa kwa wananchi walio
kwenye sekta isiyo rasmi. Kushoto ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka SSRA,
Bw. Onorius Njole.
Mkurugenzi
wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii (SSRA), Bw. Onorius Njole akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam kuhusu Program maalum ya kutoa elimu ya hifadhi
ya jamii kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Waratibu wa Mifuko
ya Bima ya Afya ya Jamii nchini kote. Zoezi hilo linaenda sambamba na
usajili wa mifuko hiyo. Kulia ni Mkuu wa Uhusiano na Uhamasishaji wa
SSRA, Bi. Sarah Kibonde na kushoto ni Afisa Uhusiano Ally Masaninga.
Baadhi
ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa SSRA uliofanyika leo
jijini Dar es Salaam ambao ulilenga kuufahamisha umma maboresho
mbalimbali katika sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
……………………………………………………………………………………………………………….
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali kupitia Mamlaka ya
Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imejizatiti
kupanua wigo na kuboresha huduma za hifadhi ya jamii hasa kwa kundi la
watu walio kwenye sekta isiyo rasmi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi
wa Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA), Bw. Onorius Njole wakati akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mpango Maalum wa kutoa huduma ya
hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi maarufu kama Informal Sector
Scheme ambayo inajumuisha waendesha bodaboda, bajaji na mama lishe.
Bw. Njole alisema kuwa katika
kuhakikisha watanzania wote wananufaika na huduma za hifadhi ya jamii,
SSRA inafanya tafiti mbalimbali na kuhamasisha Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii kubuni mafao mbalimbali yanayolenga kuwafikia wananchi wote walio
kwenye sekta isiyo rasmi.
Ili kufanikisha hilo, mwaka 2015
SSRA ilifanya utafiti katika sekta ya usafirishaji na kubaini kuwa
asilimia 83 ya waendesha vyombo vya usafiri mijini wakiwemo waendesha
bodaboda wako tayari kuchangia kwa hiari katika Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii.
“Kutokana na matokeo hayo mamlaka
ilipendekeza kuanzishwa kwa Mpango Maalum ujulikanao kama Informal
Sector Scheme ambapo watu waliojiajiri kwenye sekta isiyo rasmi watapata
nafasi ya kunufaika na huduma ya hifadhi ya jamii.” Alisema Njole.
Njole aliongeza kuwa tayari
baadhi ya mifuko imekwishaandaa mafao maalum yanayowalenga waendesha
bodaboda, bajaji, daladala na mama lishe ambao watapata fursa ya
kuchangia kiasi kidogo kila siku kulingana na kipato chao ili kupata
huduma za hifadhi ya jamii kama vile akiba ya uzeeni, matibabu na
mikopo.
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha
Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Bi. Sarah Kibonde alieleza kuwa
mamlaka hiyo inaendelea na zoezi la kutambua na kusajili Mifuko yote ya
Bima ya Afya ya Jamii (CHFs) kwa lengo la kuboresha huduma na kuimarisha
mfumo wa utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Pia Bi. Sarah alisema kuwa SSRA
imeandaa program maalum kwa ajili ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa
Wakurugenzi wa Halmashauri na Waratibu wa Mifuko ya Bima ya Afya ya
Jamii nchini kote na zoezi hilo linaenda sambamba na usajili wa mifuko
hiyo kwa mujibu wa Sheria ya SSRA, Sura ya 135.
“Program hii imeanzia Kanda ya
Kati ambako ilihusisha Wilaya 27 na jumla ya CHF 5 zilisajiliwa na
nyingine 22 zinakamilisha taratibu za usajili. Zoezi hili linatarajiwa
kuendelea Juni 22 kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambako jumla ya CHF
25 zinatarajiwa kusajiliwa.”
Sambamba na program hiyo Serikali
kupitia Wizara ya Afya na Wizara yenye dhamana ya masuala ya hifadhi ya
jamii na SSRA inafanya mapitio ya mfumo wa usimamizi wa Mifuko ya Bima
ya Afya ya Jamii (CHF) ili kupata mfumo utakaoweza kutoa huduma ya afya
kwa watanzania wote.
EmoticonEmoticon