KATIBU MKUU UJENZI ATAKA TAARIFA NDANI YA SIKU MBILI UHARIBIFU WA FLOW METER NA CAMERA BANDARINI

May 18, 2016

FL1 
Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam Hebel Mhanga( wa pili kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho( wa pili kulia) kuhusu ufanyaji kazi wa mifumo ya kuendesha mita ya kupimia mafuta (flow meter) uliojengwa eneo la Kwa Mwingira Mji Mwema Kigamboni Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na katibu Mkuu huyo leo Mei 18,2016.
FL2 
Meneja Mradi /msimamizi wa Ujenzi wa mradi wa Mita za kupimia mafuta Mhandisi Mary Mhayaya (kulia) akitoa maelezo kwa  Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho (kushoto) kuhusu mfumo wa kompyuta wa mita ya kupimia mafuta unavyofanya kazi kwa kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa wa utendaji kazi wa mita hiyo leo Mei 18,2016.
FL3 
Habour Master Kapteni Abdul Mwengamuno kutoka Mamalaka ya Bandari ya Dar es Salaam(kulia) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho (kushoto) hatua za kuzingatia wakati wa upakuaji wa mafuta kutoka kwenye meli mpaka kwenye mita za kupima mafuta ambapo mafuta hayo huchujwa kuondoa uchafu kwa kupitia mitambo maalum iliyofungwa kwenye mita hiyo.
FLO4 
Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho akipanda ngazi kuelekea kwenye pambu na valvu zilizofungwa kwenye mita ya kupimia mafuta(Flow Meter) wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua utendaji kazi wa mita hiyo leo Mei 18,2016.
FLO5 
Meneja Mradi /msimamizi wa Ujenzi wa mradi wa Mita za kupimia mafuta Mhandisi Mary Mhayaya(kushoto) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho (wa pili kushoto) kuhusu hitilafu iliyojitokeza katika moja ya valvu zilizoko kwenye  mita hiyo, upande unaoendeshwa  kwa kutumia  mfumo wa digitali  hali iliyosababishwa na mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.Mita hiyo sasa inatumia mfumo wa analojia na  hatua ya urejeshaji wa valvu hiyo katika hali yake ya awali inafanyiwa kazi na mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga mita hiyo leo.
FLO6 
Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho ( wa pili kulia) akitoa maagizo kwa Mamlaka ya Bandari kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza ikiwemo hitilafu ya kamera za ulinzi na baadhi ya valvu kwenye mita ya kupimia mafuta na kuwasilisha taarifa ofisi kwake Jumatatu Mei 23 namna ya watakavyoshughulikia mapungufu yaliyojitokeza.
FLO7 
Meneja Mradi /msimamizi wa Ujenzi wa mradi wa Mita za kupimia mafuta Mhandisi Mary Mhayaya akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho (mwenye Kaunda suti) kuhusu ufanyaji kazi wa mtambo unaochuja mafuta kwa lengo la kudhibiti na kuzuia mafuta machafu kuingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam leo Mei 18,2016.
FLO8 
Mita ya Kupimia Mafuta (Flow Meter) iliyojengwa eneo la kwa mwingira, mji Mwema Kigamboni  Jijini Dar es salaam . Utaratibu wa kujenga uzio na paa kufunika mtambo huo unaendelea kupitia mkandarasi aliyepewa jukumu la kujenga mradi huo ili kuhimarisha ulinzi na usalama wa mita hiyo.( Picha na Raymond Mushumbusi na Aron Msigwa -MAELEZO)
………………………………………………………………………………………………………………………………
Na Lorietha Laurence- Maelezo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano(Uchukuzi) Mhandisi Dkt. Leornad Chamuriho ameutaka uongozi wa Bandari unaosimamia Mitambo ya Kupimia Mafuta Nchini (Flow Meter) iliyoko Kigamboni kutoa taarifa ya kuharibika kwa mitambo hiyo ndani ya siku mbili.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu huyo alipofanya ziara ya kushtukiza katika mitambo hiyo  na kubaini upungufu katika vitendea kazi ikiwemo kamera ya kufuatilia mwenendo bandarini hapo, “valvu, sloptank” na kuchelewashwa kwa ujenzi wa kufunikwa kwa mitambo.
“Ifikapo Jumatatu nipatiwe taarifa kuhusu matengenezo ya vifaa hivi, hatua zilizochukuliwa na mnieleze lini ukarabati wake utakamilika” alisema Dkt. Chamuriho.
Aidha, aliongeza kuwa dhumuni la Serikali ni kuhakikisha vifaa hivyo vinafanya kazi ili kulinda mapato yatokanayo na mafuta yanayoingia nchini ili Serikali ipate kodi halali na hivyo kuongeza mapato ya nchi na kuondoa malalamiko kwa wateja.
Naye Meneja Mradi wa Mitambo ya Kupimia Mafuta kutoka Mamlaka ya  Bandari nchini Mhandisi Mary Mhayaya ameeleza kuwa uharibifu wa vifaa hivyo umesababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na tayari vifaa hivyo vimeanza kufanyiwa kukabarati.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Hebel Mhanga amesema ofisi yake inajukumu la kuhakikisha inatoa huduma sahihi kwa wateja wanaotumia mitambo hiyo iliyopo bandarini  hapo na Serikali inapata mapato kulingana na huduma iliyotolewa.
Mradi wa Mitambo ya Kupimia Mafuta nchini  ipo katika majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo tayari meli tatu zimefanyiwa majaribio ya upakuaji wa mafuta huku moja ikiwa imefanyiwa vipimo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »