Jaji
Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy Mutunga (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa
kusikiliza na kuamua mashauri mengi yanayopelekwa mahakamani. Kushoto
ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman na Kulia ni Jaji
Kiongozi Mhe. Shaan Lila.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumzia ujio wa Jaji Mkuu wa Kenya.
…………………………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy
Mutunga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa
kusikiliza na kuamua mashauri mengi yaliyopelekwa mahakamani kwa mwaka
wa sheria uliopita wa 2015 na kutoa wito kwa watendaji wa Mahakama ya
Tanzania kuendelea kufanya vizuri licha ya changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo.
Jaji Mkuu wa Kenya ametoa pongezi
hizo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mara baada ya
kukutana na kuongea na Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani
Tanzania kufuatia mwaliko alioupata wa kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya
Sheria nchini yatakayofanyika Februari 4 mwaka huu.
Mhe. Dkt. Mutunga amesema kuwa
nchi ya Kenya mpaka sasa ina mashauri yapatayo 300,000 ambayo bado
hayajaamuliwa na kuongeza kuwa asilimia 5 ya wananchi wa Kenya ndio
hupeleka mashauri yao Mahakamani huku asilimia 95 iliyobaki wakitafuta
ufumbuzi wa kesi zao nje ya Mahakama.
“Ni kweli Tanzania mnafanya vizuri
katika katika kusikiliza mashauri kwa haraka, asilimia 95 ya Wakenya
hutafuta ufumbuzi wa kesi zao kwa viongozi wa kidini na Kimila kutokana
na baadhi yao kukosa fedha za kutosha za kufuatilia na kugharamia kesi
zao” Amesema.
Ameongeza kuwa Mahakama ya Kenya
kwa mwaka huu 2016 imejipangia malengo ya kuhakikisha kuwa inasuluhisha
mashauri yote ndani ya mwaka mmoja ili kuongeza ufanisi na imani kwa
wananchi.
Ameeleza kuwa Tanzania ina jambo
la kujifunza kutoka Kenya kufuatia mageuzi ya Katiba iliyoyafanya mwaka
2010 hususan kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo na nafasi ya Mahakama
kwenye Katiba Mpya ambayo Tanzania inaendelea na mchakato wake.
Akizungumzia mageuzi hayo ambayo
tayari Kenya imeyafanya kufuatia kuwepo kwa Katiba mpya Mhe. Mutunga
amesema kuwa ni pamoja kupungua kwa madaraka ya Rais katika kuteua
Majaji, na nafasi za Majaji kutangazwa na watu kupeleka maombi na sifa
zao kujadiliwa ambapo wananchi huruhusiwa kutoa maoni kwa Tume ya
Mahakama ya Kenya kuhusu majaji hao kabla ya kuapishwa.
Aidha, ameeleza kuwa Watanzania
wana kila sababu ya kujivunia umoja na mshikamano uliopo ambao
umesababishwa na waasisi wa taifa hilo huku akibainisha kuwa majadiliano
na upatikanaji wa Katiba Mpya utafanywa na Watanzania wenyewe kwa kuwa
Watanzania ni walimu na mfano wa kuigwa katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumzia ujio wa Jaji Mkuu wa
Kenya amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imenufaika na ujio wake kwa kuwa
iko kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo huwakutanisha wadau
mbalimbali wa sharia kujadili changamoto na mafanikio ya Sekta ya Sheria
nchini.
Amesema kuwa kufuatia ziara ya
Jaji Mkuu wa Kenya Mahakama ya Tanzania imejifunza masuala mbalimbali
ambayo ni muhimu katika ufanisi wa shughuli zake ikiwemo Maslahi ya
Watumishi wa Mahakama, Jukumu la Mahakama kutafsiri Katiba kwa kuangalia
historian a uchumi pia kuazima baadhi ya hukumu zilizotolewa nchini
Kenya kama ushauri.
Aidha, amebainisha kuwa Mahakama
ya Tanzania inao wajibu wa kuendelea kuongeza uwazi katika upatikanaji
wa watendaji wake wenye nia ya kuwatumikia wananchi na kuboresha njia za
kuwapata majaji.