Na Mwandishi wetu,
Shirika la Majisafi na Majitaka Jijini Dar es
Salaam (Dawasco), imenasa wizi mkubwa wa Maji katika nyumba tano ambazo
zimeunganishiwa huduma ya majisafi kinyume cha utaratibu maeneo ya Tabata
Magengeni, nyumba hizo zinamilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake halikuweza
kufahamika mara moja, nyumba hizo zimepangishwa kwa familia tano tofauti
(Apartments).
Akizungumzia tukio hilo katika operesheni ya mtaa
kwa mtaa ya kuhakiki matumizi sahihi ya Maji kwa wateja wa majumbani, Meneja wa
Dawasco Tabata, Bi. Victoria Masele, alisema kuwa amebaini wizi huo baada ya
kuona bili ya mwezi inayokuja haiendani na matumizi halisi ya Maji, hivyo
wakaamua kufanya uchunguzi na kubaini kuwa mteja alikuwa amejiunganishia huduma
ya Maji kinyume cha taratibu.
“Msoma
mita wetu alikuwa na wasiwasi sana na matumizi ya Maji ya hizi nyumba, kwa
sababu bili ilikuwa ndogo ukilinganisha na idadi ya familia zinazoishi kwenye
hizi nyumba, ndipo tukaamua kufanya uchunguzi wa kina na kukuta mteja
amejiunganishia laini 3 za Maji, laini 1 ikiwa imepita kwenye mita, 2
hazijapita kwenye mita, zimeelekezwa kwenye kisima na baadaye Maji yanasukumwa
na kujaza matenki 5 ya lita 10,000, na lingine la lita 6000”
“Baada
kunasa wizi huo, tuliwasiliana na meneja wa nyumba hizo ambaye hakuwepo eneo la
tukio, na kudai kuwa hajui chochote kuhusiana na wizi huo wa Maji kutokana na
kuishi mbali na nyumba hizo na kwamba wizi huo inawezekana wa wapangaji
wenyewe, lakini aliahidi kufika katika ofisi zetu za Dawasco kumaliza tatizo
baada ya wapangaji kushindwa kutupa ushirikiano” alisema Bi. Masele
Hadi taarifa hizi zinakwenda mtamboni, meneja wa
nyumba hizo alifika katika ofisi za Dawasco Tabata na kufanya mazungumzo na
Meneja wa kituo, na kutakiwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi milioni 5.3.
DAWASCO inaendelea kutoa rai kwa wananchi wote
kuwafichua wezi wa Maji kwa kuwa wanasababisha wateja halali kukosa huduma ya
Maji kwa wachache kujiunganishia huduma kinyume na taratibu, hivyo mwananchi
yeyote ambaye amejiunganishia Maji kinyume cha taratibu na ambaye hana huduma
ya Maji afike katika ofisi yoyote ya Dawasco iliyopo karibu yake ili
aunganishiwe huduma ya Maji kihalali.
EmoticonEmoticon