Na Asteria Muhozya
…………………………….
Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo ameiaigiza Kampuni ya Uendelezaji
Jotoardhi Tanzania (TGDC Ltd) kuwa ifikapo June 2016, iwe imeanza
kuchoronga mashimo 3 katika eneo la Ziwa Ngozi ikiwa ni hatua ya mwisho
inayohitajika kabla ya kuanza kujenga mitambo ya kuzalisha jotoardhi.
“Utafiti muhimu
umekamilika. Joto la maji ni kubwa, 230-250C linalokidhi uzalishaji wa
umeme. Hiki kitakuwa ni chanzo kipya muhimu cha umeme jadidifu”
,alisema Prof. Muhongo.
Ameongeza kuwa, jambo
hilo haliwezi kuendelea kusubiri kutokana na mahitaji ya nishati hiyo
nchini ikizingatiwa kuwa, Tanzania inapitiwa na Bonde la Ufa kwa kiasi
kikubwa.
“Tayari wenzetu Kenya na
Ethiopia wamepiga hatua kubwa katika nishati hii lakni kwa upande wetu
hatuna megawati hata moja kwa hili lazima tuchukue hatua tutoke hapa
tulipo. Hakuna kusubiri anzeni na Ziwa Ngozi” amesema Muhongo.
Prof. Muhongo aliitaka
Kampuni hiyo kuongeza nguvu katika eneo lenye viashiria vya jotoardhi
la Ziwa Ngozi kutokana na kuwepo maendeleo makubwa ya kitafiti
ikilinganishwa na maeneo mengine yenye viashiria kama hivyo ikiwemo eneo
la Mbaka lililopo Wilaya ya Rungwe.
“TGDC tunataka umeme wa
jotoardhi, wananchi wanataka umeme, hawatakuwa kusikia maneno, ifikapo
Mwezi juni na mimi nitakwenda Ngozi kuangalia mmefikia wapi na kama
hakuna maendeleo tutabadilisha timu ya wataalamu”, alisisitiza Prof.
Muhongo.
Akizungumzia kuhusu
fedha za miradi, Prof. Muhongo alieleza kuwa, nchi nyingi duniani
hazitegemei fedha za Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya nishati na
ndiyo sababu hata Tanzania inatafuta fedha katika taasisi mbalimbali
ikiwemo kukaribisha wawekezaji ili kutekeleza miradi hiyo.
“Serikali kwa upande
wake itasaidia kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi na
ninyi kazi yenu ni kuhakikisha umeme wa jotoardhi unaanza kutumika
Tanzania kwa kuanza na Ziwa Ngozi”.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Abbas Kandoro alisema kuwa amefarijika na maelekezo aliyoyatoa
Prof. Muhongo na kuahidi kuweka nguvu kubwa katika kufuatilia suala
hilo. ” Ujio wako umetupa ari mpya katika kusimamia miradi hii kwa
sababu rasilimali zipo lakini zimekaa tu nakuahidi kasi ya ufuatiliaji
itaongezwa”,alisema Kandoro
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Rugwe ,Mwalimu Zainabu Mbusi alieleza kuwa maagizo ya Prof.
Muhongo yamekuwa faraja na kuongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo
itaongeza kasi ya ukuaji uchumi na kuifanya Tanzania kufikia lengo lake
la kuwa miongoni mwa nchi za uchumi wa Kati ifikapo 2025.
Kwa pande wake Mbunge
wa Jimbo la Busokelo, Fred Atupele alieleza kuwa, kukamilika kwa mradi
huo kutachochea kasi ya uendelezaji wa viwanda vikubwa na vidogo na
kueleza kuwa, kwa nafasi yake watachukua jukumu la kuwaelimisha
wananchi kuhusu umuhimu wa vyanzo hivyo.
Awali akieleza akieleza
Mikakati ya Taasisi hiyo, Mkurugenzi wa TGDC , Mhandisi Boniface Njombe
alisema eneo la Mbaka ni miongoni mwa maeneo ya maji moto yenye
viashiria vya nishati ya jotoardhi.
Vilevile, alieleza hivi
sasa wataalam kadhaa wamesambaa wakifanya tafiti za mwisho katika eneo
la Mbaka ili kuanisha mipasuko na maeneo ya kuchimba nishati hiyo na
kuongeza kuwa, TGDC imelenga kwa kuanza kuzalisha umeme wa jotoradhi
wa kiasi cha megawati 200 huku lengo ikiwa ni kufikia megawati 5000.
Aidha, alieleza kuwa,
mbali na kuzalisha umeme , maji moto yanaweza kutumika viwandani na
majumbani katika kukausha mazao ikiwemo kuwa kivutio cha utalii kuoga
kwa kuwa inaelezwa kuwa maji hayo yanatajwa kuwa tiba ya magonjwa ya
ngozi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopitiwa na Bonde la Ufa eneo ambalo linatajwa kuwa na viashiria vya nishati ya jotoardhi.
EmoticonEmoticon