RAIS DK JOHN POMBE MAGUFULI AKUTANA NA MAKATIBU WAKUU NA MANAIBU KATIBU WAKUU IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

November 08, 2015

  
jpm
   Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli jana asubuhi katika Ikulu ya Dar es Salaam  amefanya kikao na Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  ili kutoa uelekeo wa Serikali anayoitaka  mara baada ya  kuapishwa.
     “Nataka Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana ya ‘HAPA KAZI TU’ na viongozi kuzingatia na kukumbuka ahadi nilizotoa ili zianze kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja” Rais Magufuli amesema.
     Katika Kikao chake, Rais ametoa mwongozo na kusisitizia kuwa ni lazima kila mtendaji Serikalini kuuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge mbele kwa ufanisi zaidi.
     Katika kikao hicho Rais ameelekeza mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili atakapo teua Baraza lake la Mawaziri mambo hayo yawe tayari ili Mawaziri watakaoteuliwa waweze kuyasimamia bila kukosa.
     Mambo hayo muhimu ni kama ifuatavyo:
Kuanzia mwezi  Januari mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure bila kulipa ada, Katika jambo hili, Rais amewataka watendaji kuanza kuliwekea mikakati tayari kwa utekelezaji Suala la mikopo ya wanafunzi nalo lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi Amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo atakapolitolea suala hilo maamuzi mengine na kueleza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa  na mabalozi wa Tanzania  wanaowakilisha nchi  huko nje.
Pengine patokee jambo la dharura sana na hata hilo lazima kibali kitolewe na Rais au Katibu Mkuu Kiongozi. Badala yake Rais amewataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi wa Tanzania.
     Katika Kikao hicho, Rais amemtaka Kamishna wa TRA, Ndugu Rished Bade kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kero ndogo ndogo kwa wananchi lianze kutekelezwa kama alivyo ahidi kwa  kufanyiwa  kazi mapema  zaidi.
     Rais ameitaka TRA kukusanya mapato hayo kutoka kwa wafanya biashara wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote hapa Tanzania na kusisitiza kuwa katika Serikali hii wa kutoa maamuzi vinginevyo zaidi ya haya ni yeye Rais  ama Makamu wake.
     Rais Magufuli pia ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa kuibia Serikali  kwa watu kuongeza bei ya vitu hata kama ni vya bei ndogo kabisa katika jamii.
     “Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja”. Rais amesema, na kuwataka watendaji hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia maadili mema ya kazi.
Imetolewa na Premi Kibanga, Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi Ikulu, DAR ES SALAAM.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »