Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku, ambapo inatarajia kugawa mitungi 26,040 katika mkoa wa Tanga, Mradi huo utagharimu jumla ya shilingi milioni 455.
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Burian, tarehe 17 Desemba, 2024 ameupokea rasmi Mradi huo wa kusambaza mitungi ya gesi kwa Wananchi wa mkoa wa Tanga, ambapo mkoa unataraji kuanza zoezi la kusambaza mitungi hiyo kwa Wananchi mwezi Januari, 2025.
REA, iliingia mkataba na mtoa huduma; kampuni ya Manjis Logistic Ltd, kampuni ambayo, itahudumia wilaya 8 za Mkoa wa Tanga kwa kuuza mitungi hiyo ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500 pamoja na vifaa vyake, katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Burian, amewaomba REA kuhakikisha kuwa teknolojia za nishati safi ya kupikia, zinapatikana kwa wakati na kuwafikia Wananchi muda wote ili kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanakuwa endelevu.
Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa mkoa unaendelea kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi na aliwapongeza Wadau mbalimbali (Wakiwemo REA) wanaosaidia kampeni hiyo kwa kugawa mitungi ya gesi kwa Wananchi.
“Mradi huu unakwenda sambamba na malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034; uliozinduliwa mwezi Mei mwaka huu, ambapo lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na salama”. Alisema Dkt. Batilida.
Kwa upande wake; Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi, Advera Mijage amesema kazi ya Serikali ni kuhakikisha nishati safi za kupikia zinawafikia Wananchi wa ijijini kwa ukaribu zaidi na kwa bei nafuu na kuongeza kuwa Serikali inafanya kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.
“Kila kaya itanunua mtungi mmoja tu wa gesi. Mtoa huduma atahakikisha uhalali wa taarifa za mnunuzi kabla ya kumuuzia mtungi wa gesi. Pia atahakikisha mwananchi ambaye ameshauziwa harudii kuuziwa mtungi mwingine kwa kurekodi taarifa hizo kwa njia ya kidijitali.”Amesema, Mhandisi Mwijage.
Wilaya zitakazonufaika na usambazaji wa mitungi hiyo ya gesi ni pamoja na Bumbuli; Handeni; Korogwe; Lushoto; Mkinga; Muheza; Pangani na Kilindi.
EmoticonEmoticon