JKCI yashangaa idadi kubwa ya watu waliojitokeza Handeni

December 20, 2024

 


Na MASHAKA MHANDO, Handeni


TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeshangazwa na idadi kubwa ya watu wapatao 908, waliojitokeza wilayani Handeni kuchunguzwa afya kwa siku nne kufuatia kambi iliyowekwa na taasisi hiyo wilayani hapa.


Akizungumza mara baada ya kumalizika kambi hiyo juzi, msimamizi wa kambi hiyo Dkt Eva Wakuganda daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa taasisi hiyo alisema jana kuwa idadi hiyo ni kubwa kuliko maeneo mengi waliyokwenda kuchunguza afya za wananchi.


Alisema Handeni mjini pekee walijitokeza watu 411 na Handeni vijijini 497 na kufanya idadi yote kuwa 908 wakiwemo watoto 102 waliojitokeza kwa siku zote nne wilayani hapa hatua ambayo imewashangaza tofauti na maeneo mengine walikotoa Huduma za bure kama hizo.



"Kiukweli Handeni imevunja rekodi kati ya maeneo yote tuliyokwenda katika mikoa 16 kuchunguza wagonjwa hii ni nzuri kwasababu wananchi wanatambua umuhimu wa kutazama afya zao, lakini pia inatakiwa wananchi wasisubiri kambi za namana hii wajitoe kuchunguza afya zao kabla ya kukutwa na hali mbaya zaidi," alisema Dkt Wakuganda.


Alisema vijijini bado kunahitaji kutoa msaada kufanya kambi mara kwa mara kwasababu wagonjwa wenye uhitaji ni wengi na hawana uwezo wa kufika mjini lakini pia hawana bima na wengi wana matatizo hawajaweza kupata bahati ya kukutana na madaktari bingwa hivyo jitihada zaid kuwafikia zinahitajika.

Alisema kati ya hao wagonjwa wote wa Handeni Mjini na Vijijini ambako kambi ilikuwa katika mji wa Mkata, walikutwa na matatizo mbali mbali walipewa dawa bure na wengine wameandikiwa rufaa wafike katika hospital hiyo.


"Wagonjwa ni wengi na bado wana uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa, kambi hizi ziendelee kufanyika mara kwa mara vijijini ili kuwafikia wagonjwa pamoja na upatikanaji wa dawa kwani wagonjwa wengi hawana uwezo wa kununua dawa, wameshukuru sana kupatiwa dawa bure kutoka JKCI," alisema daktari bingwa huyo na kuongeza,


"Wagonjwa waliokutwa na matatizo ya moyo walipewa dawa bure na baadhi yao kupewa rufaa kwenda hospitali ya Jakaya Kikwete,".


Pia daktari huyo alisema wananchi waliowaona wamepata elimu ya lishe bora na kuacha ulaji mbovu wa chakula, ufanyaji wa mazoezi angalau dakika 30 hadi lisaa limoja kwa siku kuboresha afya zao, kuacha uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, kupunguza mafuta, chumvi na kupunguza uzito ili kujikinga na magonjwa ya moyo.


Kwa upande wa watoto Dkt Wakuganda aliwashauri akina mama waanze kliniki mapema wakiwa wajawazito ili kufuatiliwa afya zao mapema maana sababu nyingi za matundu katika moyo wa watoto hazijulikani na hutokea ghafla 

lakini tafiti zimeonyesha kisukari wakati wa ujauzito huleta athari mara nne zaidi, uvutaji wa bangi na sigara, unywaji wa pombe wakati wa ujauzito, magonjwa kama rubella huweza kuathiri mtoto tumboni, pamoja na historia ya magonjwa hayo katika familia na sababu nyingine nyingi 

Hivyo kuanza kliniki mapema kunasaidia kufuatiliwa mapema na kupewa ushauri.


Dkt Wakuganda alisema kambi hiyo iliyoanzishwa na Umoja wa Maendeleo Handeni (MMAHA) imetolewa na mfuko wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa Tiba Mkoba.


"Wananchi wamempongeza sana Rais Dkt Samia kwa kuanzisha mfuko huo ambao hakika umekuwa ukiwasaidia wananchi wengi wenye uhitaji nasi kama taasisi tunampongeza pia Rais kwasababu hali hairidhishi huku vijijini," alisema Dkt Wakuganda.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »