Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) inatarajiwa kuendelea wikiendi
hii kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, ikiwa
katika mzunguko wa saba timu 14 zitapambana kusaka pointi 3 muhimu.
Young Africans watawakaribisha Azam FC katika uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam siku ya Jumamosi, huku timu zote zikiwa na pointi 15
kileleni zikitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa.
Kabla ya mchezo wa Yanga dhidi ya Azam, kutakua na mchezo wa
utangulizi wa kuombea amani kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Mchezo huo utawakutanisha viongozi wa dini watakocheza dhidi ya
mabalozi wanaofanya kazi nchini, mechi hiyo itaanza saa 8:25 mchana na
kumalizika saa 9:15 alasiri.
Majimaji FC ya mkoani Ruvuma watakua wenyeji wa African Sports kwenye
uwanja wa Majimaji mjini Songea, huku Ndanda FC wakiwakaribisha Toto
African kutoka jijini Mwanza katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini
Mtwara.
Jijini Mbeya, watoza ushuru wa jijini hilo Mbeya City FC
watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine, Chama la wana Stand
United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga, huku Coastal Union wagosi wa kaya wakiwakaribisha wakata miwa
wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili kwa michezo miwili kuchezwa, Mgambo
Shooting watakua wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakwani,
huku Mwadui FC wakicheza na maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Mwadui
Complex.
Taarifa zote za TFF, Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja wa Kwanza (FDL)
ikiwemo ratiba, matokeo na msimamo, wafungaji zinapatikana kwenye
tovuti ya TFF, www.tff.or.tz