“KIPINDUPINDU CHABISHA HODI TANGA”CHAUA WATU TISA WENGINE 485 HOI HOSPITALINI”

October 29, 2015

WATU tisa wamefariki dunia huku wengine 485 wakiugua ugonjwa wa kipindupindu kutoka wilaya za Tanga,Muheza,Handeni na Korogwe zilizopo mkoani Tanga baada ya wananchi kuharisha na kutapika

Akizungumza jana,Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga,Salum Chima alisema kuwa hali hiyo imejitokeza katika sampuli zipatazo 50 zilizofanyiwa uchunguzi wa kimaabara na sampuli tatu zimebainika kuwa na vimelea vya kipindupindu.

Chima alisema kuwa mgonjwa wa kwanza alibainika Octoba 9 mwaka huu akitokea kitongoji cha Mswaha Darajani Kijiji cha Mswaha Kata ya Mswaha wilayani Korogwe Vijijini.

Alisema kuwa baada ya hapo Octoba 15 mwaka huu wagonjwa wengine waliendelea kujitokeza kutoka maeneo mbalimbali ya Halmashauri hizo ikiwemo Korogwe mji maeneo ya Kilole,Majengo,Ngombezi wakati kwa wilaya ya Handeni walipatikana wagonjwa maeneo ya Mandera,Kabuku Kwamatuku na Segera.

Aidha alisema kuwa kwa upande wa Halmashauri ya Korogwe vijijini wagonjwa waliougua ugonjwa huo walipatikana kwenye vijiji vya Mswaha na Hale wakati katika wilaya ya Muheza wagonjwa wote walipatikana eneo la Hale wilayani Korogwe Vijijini.

Chima alisema kuwa walibaini kuwa katika maeneo wanapotoka  wagonjwa wengi ni yake yanayopata huduma za maji kutoka chanzo cha maji mto Pangani pamoja na chanzo cha (Handeni Transimision Main) ambayo yanasafirisha maji kutoka mto Pangani mitambo ya Korogwe na Segera kwenda wilayani Handeni.

Alisema kuwa sampuli za maji zilizochukuliwa kutoka kwenye vyanzo hivyo  vya maji vimebaini maji hayo yamechafuliwa kwa kiwango kikubwa na vimelea vya magonjwa (E.coli) na vile vinavyosababisha kipindupindu.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kwa ngazi ya mkoa ili kuweza kukabiliana na hali hiyo,Chima alisema kuwa wameendeleza kuhimiza halmashauri kuweka makisio ya kukabiliana na majanga katika mipango kabambe ya afya (CCHPs) ikiwemo kuchukua hatua za tahadhari kupambana na mlipuko wa magonjwa ya kuharisha na kipindupindu.

Alisema kuwa sambamba na hilo wataendelea kutoa miongozo na mabango ya kuelimisha umma dhidi yakukabiliana na majanga ikiwemo milipuko ya magon jwa ya kuharisha ebola,dengue na mengineyo.

Katibu Tawala huyo alisema kuwa hatua nyengine wanakusudia kufanya ziara za usimamizi shirikishi ili kubaini namna halmamshauri zinavyotoa huduma za afya pamoja na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya mlipuko kwenye maeneo yao.

Sambamba na hilo wameweka utaratibu wa kufundisha timu za Halmashauri kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo milipuko ya magonjwa ya kipindupindu,ebola,dengue na mvua za elinino.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »