Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva (kulia),
akimkabidhi cheti cha Urais Rais Mteule wa Tanzania Dk.John Magufuli
katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam leo.
Kushoto ni Makamu wa Rais Mteule, Samia Hassan Suluhu.
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva (kulia),
akimkabidhi cheti cha Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu katika hafla
hiyo.
Rais
Mteule wa Tanzania, Dk. John Magufuli (kulia), akiwapungia mkono
wananchi wakati wa hafla hiyo ya kukabidhiwa cheti cha urais. Kutoka
kushoto ni mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira na mgombea nafasi hiyo kupitia Chama cha ADC, Chief Lutalosa Yemba.
Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi (kushoto), akimpongeza Rais Mteule wa Tanzania Dk. John Magufuli baada ya kuchaguliwa kuwa rais.
Makada
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakishangilia wakati Rais Mteule wa
Tanzania Dk.John Magufuli alipokuwa akitoka Ukumbi wa Diamond Jubilee
kukabidhiwa cheti cha urais.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo.
Rais Mteule wa Tanzania, Dk.Magufuli akimuonesha Rais Jakaya Kikwete cheti cha ushindi.
Rais Mteule wa Tanzania, Dk.Makufuli akiwa katika picha ya pamoja na wagombea urais wenzake wa vyama vingine.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva kwa kusimamia vizuri uchaguzi mkuu wa
2015.
Rais Jakaya Kikwete na Rais Mteule Dk.John Pombe Magufuli wakiwa katika picha ya pamoja na wake zao kwenye hafla hiyo.
……………………………………………………………..
Na Dotto Mwaibale
TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemkabidhi cheti cha ushindi aliyekuwa
mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk, John Magufuli baada
ya kushinda kwa kura nyingi kuliko wenzake kwenye uchaguzi uliofanyika
Oktoba 25 mwaka huu.
Aidha
wanasiasa wamemtaka Dk. Magufuli kutekeleza mambo yote ambayo ameahidi,
huku Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo Anna Mghwira., akimtaka ahakikishe
kuwa Katiba ya wananchi inapatikana ili kufanikisha dhana ya mabadiliko
ambayo yalikuwa yanatajwa na wagombea wote.
Akizungumza
kabla ya kumkabidhi cheti hicho katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa
Diamond Jubilee, Dar es Salaam leo Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu
Damian Lubuva, alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki huku
akiwapongeza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tofauti na mwaka
2010.
Lubuva
alisema katika uchaguzi huo wagombea wa nafasi ya urais ni Anna Mghwira
wa ACT, Chief Lutalosa Yemba wa ADC, Dk. Magufuli wa CCM, Edward
Lowassa wa Chadema, Hashim Rugwe wa Chaumma, Malik Kasambala wa NRA,
Elifatio Lyimo wa TLP na Fahmi Dovutwa wa UPDP.
Alisema,
tume imemtanga Dk. Magufuli kwani amefanikiwa kupata kura nyingi kuliko
wagombea wenzake ambapo walioandikishwa ni wapigakura 23,161,440,
waliopiga kura ni 15,589,639 sawa na asilimia 67,31 ya waliojiandikisha.
Alisema kura halali ni 15,193,862 sawa na asilimia 97.46, kura zilizokataliwa ni 402,248 sawa na asilimia 2.58.
Jaji
Lubuva alitangaza matokeo kuwa Mghwira amepata kura 98,763 sawa na
asilimia 0.65, ADC amepata kura 66,049 sawa na asilimia 0.43.
Dk.
Magufuli amepata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 sawa na asilimia
58.46, Lowassa amepata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97, Rungwe
49,256 sawa na asilimia 0.32, Kasambala amepata kura 8,028 sawa na
asilimia 0.05.
Wengine ni Lyimo amepata kura 8,198 sawa na asilimia 0.05, Dovutwa amepata kura 7,785 sawa na asilimia 0.05.
Kailima
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhan, alisema kura
zilizopigwa zinatoka katika majimbo ya uchaguzi 264 na kata 3,957 na
hakuna dosari kubwa ambayo ilitokea.
Alisema
katika nafasi ya ubunge majimbo yaliyofanya uchaguzi ni 256 huku
majimbo nane yakiwa hayajafanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali
ambazo ni vifo kwa wagombea na karatasi za wagombea kuwa na mapungufu.
Kailima
alisema pia kuna Kata ambazo hazijafanya uchaguzi kutokana na mapungufu
mbalimbali ambapo wanatarajiwa kufanya uchaguzi mapema iwezekanovyo.
“Mchakato
wa uchaguzi umefanyika kwa kufuata sheria hivyo tume inadiriki kusema
uchaguzi ulikuwa huru na wa haki kwani hakuna lalamiko lolote kutoka kwa
wakala,” alisema.
Alisema
kifungu cha 85 kinaipa mamlaka haki ya kutangaza matokeo hata kama
baadhi ya wagombea watagoma kusaini matokeo husika hivyo aliyetangazwa
na tume ndiye mshindi.
Mghwira
Akizungumza
baada ya tume kumkabidhi mshindi cheti, aliyekuwa mgombea wa urais
kupitia ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, alisema anakubaliana na matokeo na
kumtaka Magufuli ahakikishe kuwa anasimamia upatikanaji wa katiba.
Mghwira
alisema, iwapo anataka mabadiliko yaweze kupatikana ni jukumu lake
kusimamia upatikanaji wa katiba ya wananchi kwani ndiyo inaweza kuleta
mabadiliko sahihi kwa Tanzania ya leo.
Aidha,
alimtaka mshindi huyo wa nafasi ya urais kusimamia suala la usawa na
umoja wa kitaifa ambao utaweza kujenga nchi kufikia maendeleo sahihi
pamoja na wananchi.
“Tunahitaji
uchumi imara ili kurejesha fahari ya nchi na wananchi kwani hakuna
shaka kuwa wananchi wamekata tamaa na taifa lao jambo ambalo sio
sahihi,” alisema.
Mghwira alitumia nafasi hiyo kumkabidhi Dk. Magufuli, ilani ya chama hicho kwani ina malengo ya kuibadilisha Tanzania.
Yemba
Kwa
upande wake aliyekuwa mgombea urais, kupitia Chama cha Alliance for
Democratic Change (ADC), Chifu Litalosa Yemba, alisema anampongeza Dk.
Magufuli kwa ushindi huku akiweka bayana kuwa tangu aanze kushiriki
chaguzi uchaguzi wa mwaka huu ndio uchaguzi ambao ulikuwa huru na wa
haki.
Alisema
mapungufu ambayo yanalalamikiwa na baadhi ya wagombea yanapazwa
kuangaliwa kwa undani zaidi ili kuhakikisha kuwa hayarejei kutokana na
ukweli kuwa mchakato huo ni muhimu kwa wananchi.
Yemba
alisema, anampongeza mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa, kwa kufanya kampeni za kistaarabu pamoja na
matusi, kashfa na dharau ambazo zimejitokeza kwake.
“Tunaweza
kusema mambo mengi ila ambaye ahataki kutambua mchango wa Lowassa
katika siasa za Tanzania hasa upinzani atakuwa hajui siasa ninachoomba
Chadema na vyama vya upinzani kudumisha nguvu hii kwani hatujaweza
kupata kura zaidi ya milioni 2 tangu kuanza kwa vyama vyetu,” alisema.
Aidha,
ameweka bayana kuwa iwapo angefanya kampeni katika uchaguzi huu
angeweza kuwa mshindi wa pili lakini kutokana na uhaba wa fedha
walishindwa kufanya kampeni ila anawashukuru wananchi kwa kura ambazo
wamepata.
Jonatha
Akizungumzia
uchaguzi huo Kiongozi wa waangalizi kutoka Jumuia ya Madola, Rais
mstaafu wa Nigeria, Godluck Jonathan, alisema uchaguzi ulikuwa huru na
haki na kuzitaka nchi zingine kuiga Tanzania kwani imekuwa mfano bora.
Godluck
alisema, uchaguzi ni jambo ambalo linakuwa na changamoto mbalimbali
ambapo sio jambo rahisi kila mtu kukubaliana na matokeo lakini kwa
mtazamo wao wanaamini kuwa uchaguzi huo umefanyika vizuri.
Nchemba
Mwigulu
Nchemba ambaye ni mbunge mteule wa Jimbo la Iramba Magharibi, alisema
amefurahishwa na ushindi huo kwani Dk. Magufuli ana vigezo vyote
vinavyohitajika kwa kiongozi wa nchi.
Alisema
watanzania wajiandae kwa kupata mabadiliko sahihi ambayo walikuwa
wanayataka kwani kiongozi huyo ni mtu ambaye anasimamia uwajibikaji,
uadilifu na mchapakazi.
“Vigezo
vimetumika kumpata rais sahihi kwa maslahi ya Taifa, hivyo kilichobakia
ni watu kufanya kazi ili dhana nzima ta hapa kazi tu ionekane na
mabadiliko pia,” alisema.
Mwijage
“Huyu
ndiye chaguo sahihi kwa maslahi ya Taifa na pia naamini hata Mungu
ndiye aliyetaka tumpate Magufuli naamini mabadilikio yataanza vijijini
ili kuzuia watu kuja mijini kutafuta kazi,” alisema.
Alisema
watu wajiandae kufanya kazi kwani kasi ya kiongozi huyo mpya wa nchi
itakuwa haina mzaha hivyo wale wakaa vijiweni watambue kuwa nafasi hiyo
haipo kupitia Dk. Magufuli.
Madabida
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan
Madabida, alisema ushindi huo wameupokea kwa furaha pamoja na ukweli
kuwa yalikuwa ndio matarajio yao.
“Sisi
hatukuwa na shaka kuhusu ushindi huo lakini pia mgombea wetu ni mtu
mzuri sana katika utendaji naamini kuwa wananchi wamemuelewa hivyo
watarajie kuona mabadiliko ya kweli,” alisema.
Madabida
alisema vyama vya upinzani vilikuwa vinatumia nguvu ya hali ya juu
kuhakikisha kuwa vinashinda lakini kutokana na mikakati yao wamefanikiwa
kuibuka kidedea.
Kuhusu
majimbo mengi ya mkoa wake kuchukuliwa na vyama vya upinzani alisema
hayo ni maamuzi ya wananchi lakini wao kama uongozi walifanya kila
linalowezekana kufanikisha ushindi.
Aidha,
alikanusha taarifa za kuwa wameshindwa kutokana na yeye kumuunga mkono
Lowassa wakati yupo CCM na kuwa hakufanya kampeni na kuweka bayana kuwa
alikuwa anamuunga mkono wakati huo ila kwa sasa alikuwa na Magufuli.
Katika
hafla hiyo ya kumkabidhi cheti cha ushindi Dk. Magufuli na Makamu wake
Samia Suluhu Hassan, pia Rais Jakaya Kikwete, alishiriki, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, Spika wa Bunge Anne Makinda, Rais wa Awamu ya Pili, Ally
Hassan Mwinyi, Mawaziri Wakuu wastaafu na viongozi wengine walihudhuria
pamoja na wananchi na wanachama wa CCM.
EmoticonEmoticon