WAJASILIAMALI WAHIMIZWA KUTUMIA INTERNET KUTANGAZA BIASHARA ZAO

September 06, 2015

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Bw. Salim Maulidi Salim akimkabidhi picha ya mlango wa asili ya Zanzibar, Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi jijini Birmingham, Bw. Prince Kateka II ikiwa ni ishara ya kukaribishwa Zanzibar.
Wafanyabiashara wamehimizwa kutumia mtandao wa internet kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa kwa kuwa njia hiyo ni nafuu na inawafikiwa watu wengi kwa haraka. Hayo yalibainishwa na Bw. Dickson Inachee, Raia wa Uganda alipokuwa anatoa mada katika kongamano la siku mbili la Watanzania wanaoishi Uingereza lililomalizika jijini Birmingham siku ya Jumamosi tarehe 05 Septemba 2015. 
Bw. Inachee alieleza kuwa, kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya watu milioni 9.3 wanatumia internet nchini Tanzania. Kati ya hao watu milioni 2.4 wanatumia mtandao wa face book, hivyo ukitangaza katika face book, tangazo lako litawafakia watu wengi kuliko kutumia vyombo vilivyozoeleka kama magazeti. 
Aliendelea kueleza kuwa tangazo katika face book linatozwa Dola moja ya Marekani na kwa Tanzania litawafikia watu milioni 2.4 lakini tangazo hilo hilo ukilitoa katika gazeti linalopendwa sana nchini Tanzania utatakiwa kulipa Dola 300 na litawafikia watu elfu 50 tu. 

Bw. Inachee alimalizia mada yake kwa kusisitiza kuwa, endapo wajasiliamali nchini Tanzania wanataka kufanya biashara kwa kutumia mbinu mpya za kibiashara, basi hawana budi kutumia internet kutangaza bidhaa zao kwa kuwa njia hiyo itawaondolea mzigo wa kulipa fedha nyingi katika vyombo vilivyozoeleka sanjari na kuwafikia watu wengi zaidi.
Bw. Anthony Chaula akiwasilisha mada
Katika hatua nyingine, wanadiaspora walioshiriki kongamano hilo, wameridhishwa na hatua ya Serikali ya kuwapa hadhi maalum katika Katiba inayopendekezwa.

 Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Bw. Anthony, Chaula kutoka Idara ya Uhamiaji alisema kuwa Katiba inayopendekezwa itakapopitishwa, wanadiaspora watapewa hadhi maalum tofauti na ilivyo sasa ambapo wanaonekana kama wageni wengine.
Wakati wa kongamano hilo, baadhi ya Watanzania wanaoishi Uingereza walitumia fursa hiyo kutangaza shughuli zao za kibunifu wanazofanya katika nchi hiyo. Bw, Ayoub Mzee alizindua rasmi progaramu yake inayoitwa AITV APP. Programu hiyo inamwezesha mteja, kwa kutumia simu ya mkononi au kifaa kingine chenye internet kuangalia vituo takriban vyote vya televisheni vya Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa gharama ya Dola za Marekani sita kwa mwezi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo yas Nje, Balozi Liberata Mulamula aksalimiana na Bw. Ayoub Mzee kabla ya kuzindua programu ya AITV APP.
Mtanzania mwingine Bw. Mediremtula ameanzisha kampuni inayojihusisha na utengenezaji wa tablet. Anasema aina ya tablet anayotengeneza inafanya vizuri kibiashara katika nchi za Uingereza na Urusi na hivi sasa yupo katika mchakato wa kutengeneza aina nyingine ya tablet kwa ajili ya Tanzania.
Katika masuala ya sanaa hasa ya uigizaji wa filamu, Watanzania wa Uingereza hawakuachwa nyuma. Kuna Watanzania wamecheza filamu ijulikanayo Goingbongo. Filamu hiyo imeigizwa katika viwango vya kimataifa na walioafanikiwa kuiangalia wamethibitisha kuwa ni ya kimataifa kweli.
Kongamano hilo lilifungwa rasmi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais- Zanzibar, Bw. Salim Maulidi Salim ambaye alisisitiza umuhimu wa wanadiaspora kuwekeza nyumbani kwa madhumuni ya kukuza uchumi na kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira kwa jamaa zao.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Peter Kallaghe akitoa cheti cha kutambua mchasngo wa mmoja wa wadhamini wa kongamano. Na Ally Kondo, Birmingham

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »