Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa
michezo nane kuchezwa kwa siku za jumamosi na jumapili katika viwanja
nane tofauti nchini ikiwa ni mzunguko wa tatu tangu kuanza kwa ligi hiyo
mwishoni mwa wiki iliyopita.
Jumamosi mabingwa watetezi wa kombe hilo klabu ya Young Africans
watakuwa wenyeji wa JKT Ruvu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam, Chama la Wana Stand United watawakaribisha Wana Kimanumanu
African Sports katika dimba la Kambarage mjini Shinyanga.
Jijini Mbeya kutakua na mpambano wa wenyeji wa mji huo (Mbeya Derby)
kati ya Tanzania Prisons watakapokuwa wakipambana na Mbeya City katika
uwanja wa Sokoine jijini humo, huku Maafande wa Mgambo Shooting
wakiwakaribisha Wana Lizombe Majimaji FC kwenye uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili kwa michezo minne kuchezaw, Simba SC
watawakaribisha Kagera Sugar kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam, huku Mwadui FC wakiwa wenyeji wa Azam FC katika uwanja wa Mwadui
Complex mjini Shinyanga.
Wakata miwa wa Turiani Mtibwa Sugar watawakaribisha Ndanda FC ya
Mtwara kwenye uwanja wa Manungu mkoani Morogoro na Wagosi wa Kaya
Coastal Union watakua wenyeji wa Toto Africans katika uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.