UJENZI WA MINARA YA MAJARIBIO YA UMEME WA KUTUMIA UPEPO NA JUA KUFANYIKA VISIWANI HUMO

August 20, 2015
       NA MASANJA MABULA,PEMBA.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa ujenzi wa minara ya majaribio ya umeme wa kutumia upepo na jua ni hatua za kukabiliana na tatizo la kukatika katika kwa nishati ya umeme visiwani humo .
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutaondoa tatizo la kukatika katika umeme .
Kauli hiyo ameitoa wakati alipotembelea ujenzi wa mnara wa umeme wa kutumia upepo na jua katika shehia ya Kiuyu Mbuyuni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba unaojengwa kwa ushirikiano kati ya SMZ na Jumuiya ya Nchi ya Ulaya (EU).
Amesema kuwa mradi huo pia utapunguza gharama za kulipia huduma hiyo na kuongeza kwamba wananchi wengi watamudu kutumia huduma hiyo na hivyo kukuza uchumi na kuongeza kipato cha familia zao .
Aidha Seif ametumia fursa hiyo kuiwataka wananchi wa shehia hiyo kushirikiana na watendaji wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili kufanikisha ujenzi wa mnara huo .
Makamo wa pili wa Rais amewataka wananchi kuwa wastahamilivu na kuacha utafiti ufanyike ili kubaini ni aina gani ya umeme unafaa na ambao hautaathiri mazingira .
Akitoa maelezo ya ujenzi wa mnara huo kwa Makamo Meneja Mradi Maulid Shirazi Hassan amesema kuwa Jumla ya minara mitano ya umeme wa Upepo na Jua inajengwa Unguja na Pemba.
Amesema kuwa Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya  (EU) imetoa jumla ya Uero milioni tatu kwa ajili ya kazi za awali za ujenzi wa minara mitano Unguja na Pemba .
Mradi huo unajengwa kwa majaribio katika maeneo ya wazi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi  utachukua miezi kumi na nane ambayo ni sawa na mwaka mmoja na baada ya hapo ripoti ya wataalamu kuwasilishwa serikalini  .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »