Wanawake waliopona Fistula CCBRT waamua kujiajiri

May 21, 2015

Baadhi ya wanawake wa kituo cha “Mabinti” kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, chini ya Hospitali ya CCBRT wakiwa darasani kujifunza elimu ya ushanoaji wa aina mbalimbali za vitu baada ya kutibiwa na kupona Fistula kupitia mradi wa matibabu unaofadhiliwa na Vodacom Foundation. Kituo hicho kinawawezesha mabinti hao kupata elimu ya kazi za mikono ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Mmoja wasichana wa kituo cha “Mabinti” aliyepata kutibiwa Fistula na kupona katika Hospitali ya CCBRT Cherry David ( kulia) akiwaonesha maofisa wa Vodacom Foundation moja ya mkoba alioushana wakati walipotembelea katika kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam kuangalia maendeleo ya wanawake hao baada ya matibabu. Kituo hicho kinawawezesha mabinti hao kupata elimu ya kazi za mikono ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Tatu Hussen wa kituo cha “Mabinti” aliyepata kutibiwa Fistula na kupona katika Hospitali ya CCBRT akionesha umahiri wa kutengeneza urembo kwenye kitambaa (screen printing) wakati maafisa wa Vodacom Foundation ambao ndio wadhamini wa mradi wa matibabu ya Fistula kupitia CCBRT walipotembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam kuangalia maendeleo ya wanawake hao baada ya matibabu. Kushoto ni Mwalimu wa kituo hicho David Mkinga, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Renatus Rwehikiza na Afisa wa Mawasiliano Abigail Ambweni (kulia). Kituo hicho kinawawezesha mabinti hao kupata elimu ya kazi za mikono ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Mratibu wa Kituo cha Mabinti Center kilichopo chini ya Hospitali ya CCBRT Bi. Katia Geurts akiwaelezea maafisa wa Vodacom Foundation shughuli zinazofanywa na kituo hicho wakati walipotembelea kituo hicho kuangalia maendeleo ya wanawake hao baada ya matibabu. Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya kupona Fistula baada ya matibabu katika Hospitali ya CCBRT ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.

Wanawake waliougua na  kutibiwa na hatimaye kupona maradhi ya fistula katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam wameamua kujikita katika sanaa ya kazi za mikono kwa lengo la kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini.

Takribani wanawake wapatao 62, chini ya mpango madhubuti ulioratibiwa na hospitali ya CCBRT, wamekuwa wakihitimu mafunzo mbalimbali ya kazi za mikono zikiwemo sanaa za ushonaji wa batiki, nguo za aina tofauti, utengenezaji wa mabegi, kofia, na  ususi katika Kituo kinachoendeshwa na hospitali hiyo kijulikanacho kama ‘Mabinti Centre’ tangu mwaka 2007.

Mratibu wa Kituo hicho, Katia Geurts aliueleza ujumbe wa wafadhili kutoka Taasisi ya Vodacom Foundation waliotembelea kituo hapo kuwa  kituo  kinatoa mafunzo mahususi kwa wakinamama waliopona baada ya kusumbuliwa na fistula.

“Wengi wao wanatoka katika familia duni, hivyo mafunzo haya wanayoyapata baada ya kumaliza matibabu ya Fistula yanakwenda kuwasaidia kujiajiri wao wenyewe warudipo makwao jambo linalowasaidia kupunguza ukali wa maisha,” alisema Geurts.

Aliongeza kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo kituo hicho huwapatia vyeti vya uhitimu vinavyotambulika, sanjari na vitendea kazi vinavyoendana na stadi stahiki aliyohitimu mwanafunzi kwa minajiri ya kuwarahisishia upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha yao.

 Mkufunzi wa Kituo hicho ambaye awali alikuwa mmoja wa waathirika wa fistula hospitalini hapo, Tatu Hussen Jane Rugalabamu, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aanze kufundisha wenzake kituoni hapo amebaini kuna idadi kubwa ya wanawake wenye matatizo ya fistula ndani ya jamii lakini waume zao wamekuwa wakiwaficha kwa dhana ya kuficha aibu.

“Kuna haja kubwa ya kuelimisha akinababa wawaruhusu wake zao wenye matatizo waje kutibiwa. Fistula kwani inatibika na wala sio tatizo la kulogwa kama wengi wanavyodhani, sisi sote hapa kwenye kituo cha mabinti tulikuwa na maradhi hayo na sasa tumepona kabisa wanawake jitokezeni,” alisema Rugalabamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Vodacom  Foundation,Renatus Rwehikiza,  baada ya kukagua shughuli mbalimbali za mafunzo zinazoendelea kituoni hapo, alisema kwa niaba ya wafanyakazi wa Vodacom na Vodafone duniani kote, wataendelea kuwasaidia akinamama wote wanaopatwa na maradhi ya Fistula hatua kwa hatua, sambamba na kuhakikisha wanazidisha kasi katika kampeni inayoendelea dhidi ya maradhi hayo.

“Tutaendelea kuwa karibu zaidi na waathirika wa Fistula kuanzia hatua ya kuwasafirisha kutoka vijijini na mikoani kwa kuwatumia fedha kupitia huduma yetu ya M-Pesa, pia tutakuwa pamoja wakati wote wa matibabu na baada ya kupona tutawaunga mkono kwenye mafunzo kama haya ili kuwaletea ustawi ulio bora kwa maisha bora kwa ajili yao na familia zao,” alisema Rwehikiza.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »