VPL KUENDELEA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara
inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaopigwa katika dimba la
Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, wenyeji timu ya Azam FC
watawakaribisha Mabingwa wapya wa ligi hiyo msimu huu timu ya Young
Africans.
Mechi hiyo no. 141 itachezeshwa na
mwamuzi wa kati Jacob Adongo kutoka Mara, akisaidiwa na washika
vibendera Frednand Chacha (Mwanza), Hellen Mduma (Dsm), huku mwamuzi wa
akiba akiwa ni Hussein Kalindo (Dsm) na Kamisaa wa mchezo huo ni Damian
Mabena kutoka Tanga.
Katika mchezo huo timu ya Young
Africans itakabidhiwa Kombe lake la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania bara msimu wa 2014/2015, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr Fennela Mkangara.
Mchezo huo wa kesho unatarajiwa
kuanza majira ya saa 11 kamili jioni, kwa saa za Afrika Mashariki na
kati ili kutoa fursa kwa wadau, wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu
nchini kujitokeza kushudia mchezo huo pamoja na shamrashamra za
kukabidhiwa kikombe.
Young Africans watakabidhiwa Kombe
la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na mgeni rasmi, huku
wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom
wakimkabidhi zawadi mchezaji bora wa mwezi Aprili Mrisho Ngasa na fedha
taslimu sh. millioni moja.
WAAMUZI WA KIKE TANZANIA KUCHEZESHA CONGO DR VS GABON
Shirikisho la Mpira wa Miguu
barani Afrika – CAF limewateua waamuzi wa kike kutoka Tanzania
kuchezesha mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia kwa
Wanawake U-20 mwaka 2016 kati ya Congo DR dhidi ya Gabon.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa
jumamosi tarehe 09.05.2015 jijini Kinshasa – Condo DR, mwamuzi wa kati
ni Jonesia Rukya, akisaidiwa na washika vibendera Dalila Jafari na
Sophia Mtongoli huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hellen Mduma.
Wakati huo huo Elizabeth Kalinga
ameteuliwa kuwa kamisaa wa mchezo kati ya Kenya dhidi ya Botswana
kuwania kufuzu kwa michuani ya Olympiki, mchezo utakaofanyika Mei 31,
2015 nchini Kenya.
NB: Alhamisi ya tarehe 07 Mei,
2015, saa 5 kamili asubuhi, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania (Taifa
Stars) Mart Nooij ataongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa
mikutano wa TFF uliopo Karume, waandishi wote wa habari mnaombwa
kuhudhuria bila kukosa.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)