Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2015/2016 bungeni mjini Dodoma leo.
Mbunge wa Kisarawe (CCM) Bw. Suleiman Jafo akichangia mjadala wa bajeti ya wizara ya uchukuzi leo bungeni mjini Dodoma.
…………………………………………………………….
Na Fatma Salum – Maelezo
Serikali kupitia Wizara ya
Uchukuzi imesema inakaribisha wawekezaji binafsi kwenye miradi
mbalimbali ili kuboresha sekta za uchukuzi na hali ya hewa hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Uchukuzi Mhe. Dkt. Charles Tizeba wakati akijibu hoja mbalimbali za
wabunge zilizowasilishwa kwenye mjadala wa bajeti ya wizara hiyo leo
bungeni mjini Dodoma.
“Serikali inawakaribisha
wawekezaji binafsi kuwekeza kwenye miradi ya kuboresha miundombinu ya
uchukuzi na hali ya hewa kwa kuwa Serikali peke yake haiwezi kukamilisha
miradi yote bila ya ushirikiano na wengine”
Dkt. Tizeba alisema Serikali ina
mipango madhubuti ya kuboresha miundombinu nchini ikiwemo reli, bandari
na barabara na kupitia dhana ya ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi
(Public Private Partnership) itaweza kufanikisha mipango hiyo kwa
ufanisi na kwa wakati.
Aidha Dkt. Tizeba aliongeza kuwa
kupitia juhudi za Serikali baadhi ya miradi ipo katika hatua za awali
ikiwemo uboreshaji wa viwanja vya ndege 11 kwenye mikoa mbalimbali
nchini ambapo wataalamu wameshafanya upembuzi yakinifu (Feasibility
Study) na fedha zikipatikana vitafanyiwa matengenezo mara moja.
Akizungumzia upanuzi wa bandari
ya Dar es Salaam Dkt. Tizeba alibainisha kuwa taratibu za kumpata
mzabuni zinaendelea na akipatikana ujenzi wa gati namba 13 na 14 za
bandari hiyo utaanza.
Leo Waziri wa Uchukuzi Mhe.
Samuel Sitta aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya
wizara hiyo kwa mwaka 2015/2016 ambapo bunge lilikubali kupitisha zaidi
ya shilingi bilioni 452.9.
EmoticonEmoticon