Na Lorietha Laurence-Maelezo
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa Kushirikiana na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia
Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) itaadhimisha wiki ya Ukombozi wa
Bara la Afrika Mei 25 hadi 29 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO, Bw. Assah Mwambene ,amesema
maadhimisho hayo yanatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe.
katika ufunguzi huo, Mkurugenzi ameeleza kuwa maadhimisho hayo
yatatanguliwa na uzinduzi wa Mradi wa Nyaraka za Urithi wa Tanzania
(TAHAP) ikiambatana na maonyesho ya picha ya kumbukumbu mbalimbali
zinazoelezea ukombozi wa bara hilo.
“Mradi wa nyaraka za urithi wa Tanzania unatarajia kuweka na
kutunza kumbukumbu mbalimbali zinazohusu ushiriki wa Tanzania katika
harakati za zinazohusu ukombozi wa nchi za Bara la Afrika” alisema
Bw.Mwambene.
Naye Mshauri Mkuu wa masuala ya Uhifadhi wa Nyaraka kutoka
UNESCO, Bw.Philippe Roisse ameeleza namna shirika hilo lilivyojidhatiti
katika kuhakikisha kumbukumbu hizo zitakavyohifadhiwa kwa usahihi na
manufaa ya kizazi kijacho.
“UNESCO imeazimia kusimamia suala hili la uhifadhi wa nyaraka za
kumbukumbu Barani Afrika kuhusu harakati za ukombozi na hasa
ukizingatia shirika hili limefikisha miaka 17 katika kutoa huduma”
Alisema Bw. Roisse.
Kwa Upande wa Mshauri Mwelekezi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere,
Dkt. Dinah Mbaga ameeleza kuwa mchango wa Tanzania katika ukombozi wa
Afrika ni muhimu sana kwa kizazi cha sasa, na kuongeza kuwa ni muhimu
kukumbushana.
Aidha, Mshauri kutoka UNESCO Bw. Daniel Ndagala, ameongeza kwa
kueleza kuwa mradi wa uhifadhi wa kumbukumbu mbalimbali na nyaraka za
urithi ni chombo muhimu sana katika utekelezaji wa utambuzi wa juhudi za
Tanzania kwa nchi za Bara la Afrika.
Wiki ya maadhimisho ya Ukombozi wa Bara la Afrika utaenda
sambamba na midahalo mbalimbali ikiwemo, mdahalo wa mchango wa vyama vya
siasa katika harakati za ukombozi, Mchango wa wanajeshi katika harakati
za ukombozi
Mingine ni mchango wa wanawake katika harakati za ukombozi,
mchango wa wasanii na watunzi na mchango wa vyombo vya habari yote
ikilenga suala zima la harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa
kufungwa na mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni
naMichezo, Mhe. Dkt. Fenella Mukangara.
EmoticonEmoticon