KAVUMBANGU AOTA MBAWA YANGA SC, ASAINI MKATABA MPYA AZAM FC

May 11, 2015

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
DIDIER Kavumbangu (pichani juu) ataendelea kuichezea Azam FC kwa mwaka mwingine mmoja, maana yake lile dili kurejea Yanga SC limekufa kifo cha kawaida.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amesema kwamba Mrundi huyo ameongeza Mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo.
“Ni kweli tumemuongezea Mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji wetu, Didier Kavumbangu, hii ni kutokana na kuvutiwa na kazi yake nzuri katika msimu wake wa kwanza,”amesema Kawemba.
Kabumbangu alisaini mwaka mmoja msimu huu kutoka Yanga SC, lakini mwishoni mwa msimu kukaibuka tetesi anarejea Jangwani.
Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm ni shabiki mzuri wa Kavumbangu na ni kweli alitamani kufanya kazi tena na mkali huyo wa mabao.
Hata hivyo, Azam FC baada ya kuvutiwa na shughuli ya Mrundi huyo kwa msimu aliowatumikia, wameamua kuongeza naye Mkataba.
Katika msimu wake mmoja tu wa kwanza Azam FC, Kavumbangu ameifungia timu hiyo mabao 17 katika mechi 36 za mashindano yote, kati ya hato, 11 katika Ligi Kuu.
Wakati akiwa Yanga SC, Kavumbangu aliifungia timu hiyo mabao 31 katika mechi 63 za mashindano yote ndani ya misimu miwili.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »