Mtandao wa waandishi kupitia mitandao nchini, Tanzania Bloggers Network
(TBN) tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya
Mrisho Kikwete kutumia mamlaka yake vyema kwa kutokupitisha muswada wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano
mitandaoni.
Muswada wa sheria ya makosa ya
Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa
kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na kuweka utaratibu wa
upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kieletroniki na masuala
mengine yanayohusiana na hayo.
MUSWADA WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAONI, 2015
Umoja huu (TBN) ulishtushwa na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali kupitisha Muswada wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 kwa hati ya dharura kitendo ambacho
hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado ni kitu kipya nchini hivyo
tulihitaji maridhiano na wadau na elimu kati ya raia na Serikali ili
wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia mitandao na yapi yanakubalika.
Kimsingi TBN haipingi Tanzania
kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba Serikali
kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na wanamitandao ya jamii
ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana kukandamiza uhuru wa
vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na sheria isiyo na viashiria
kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea habari.
Hali kadhalika tulishuhudia
watetezi wa haki za binadamu pamoja na wawakilishi wa watumiaji wa
Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu zenye uzito za kwanini sheria
hii isipite kwa hati ya dharura na kuhoji kwanini sheria hii ipite kwa
dharura bila ya kupata majibu.
Muswada huu ambao kati ya makosa
mengi uliyonayo kubwa moja wapo ni majukumu makubwa aliyopewa Mkuu wa
Kituo chochote cha Polisi kuwa na uwezo wa kupekuwa na kuchukua
vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la uhalifu unaohusu mtandao.
Swali ni kuwa kwanini polisi apewe mamlaka ya kumsulubisha mtuhumiwa
katika hatua ya mwanzo bila uthibitisho wa sahihi?
Mbali na hapo, sisi kama waandishi
ulimwenguni kote tunatakiwa kufuatilia maadili ya kazi zetu. Maadili ya
mwandishi yeyote yule ni kutunza usiri wa chanzo cha habari yake pale
inapotakiwa lakini katika sheria hii sisi kama bloggers, sheria hii inakiuka hili kwa kutulazimisha kutaja vyanzo vya habari.
Kupitia sheria hii, bloga yeyote
yupo hatarini kutokana na kwamba sheria inaainisha ni kosa la jinai
kutoa ujumbe unaoweza kumuudhi mtu kihisia.
Aidha, tunamuomba Mheshimiwa Rais pia asipitishe Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013.
Muswada huu unavinyima uhuru
vyombo vya habari vinavyotangaza takwimu mbalimbali. Kama ilivyo Ibara
ya 7(4) ‘‘Chombo chochote cha habari ambacho kinachapisha taarifa za
kitakwimu za uongo au upotoshaji, au kinatangaza kipindi chochote
kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa ambayo imefanywa au
inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi wasishiriki kwenye
shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na maafisa wa
Ofisi, kinatenda kosa.’’
Hii iki maanisha kuwa hata blog
zetu ziko hatarini kuelekea katika kulazimika kufanya kazi za kuisifia
serikali na kutangaza takwimu zilizopitiwa na serikali tu, jambo ambalo
litaharibu ukuaji wa uhuru wa habari nchini.
Tunamkumbusha mwananchi wa kawaida
anayetumia mtandao wa intaneti kuwa hayuko salama kwani sheria hii
inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa taarifa za wateja wake jambo
ambalo linahatarisha uhuru wa kutoa na kupokea habari.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
IMETOLEWA NA;
Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network-TBN)
EmoticonEmoticon