TUKISHIRIKIANA TUTAOKOA MAISHA YA AKINA MAMA WENGI NA WATOTO

March 10, 2015

Balozi Tuvako Manongi Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa akizungumza wakati wa uzinduzi wa onyesho la picha lililoandaliwa kwa ubia baina ya Wakilishi za Kudumu za Italia na Tanzania. Onyesho hilo linahusu huduma za afya ya mama na mtoto zinazotolewa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Doctors with Africa CUAMM katika hospitali ya Tosamaganga, Mkoani Iringa. Kushoto kwa Balozi Manongi ni Balozi wa Italia katika Umoja wa Mataifa, Bw. Sebastioano Cardi na kulina ni mmoja wa Wabunge kutoka Italia anayehudhuria mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake.
Balozi Manongi akiteta jambo na Dkt. Andrea Atzori ambaye katika maelezo yake amesema taasisi hiyo ya Doctors with Africa CUAMM inampango wa kupanua huduma zake katika maeneo mengine ya pembezoni mwa Tanzania, mbali ya Tosamaganga na Mikumi.
Dkt. Andrea Atzori akiwa na Bi. Tully Mwaipopo, Afisa wa Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mara baada ya uzinduzi wa onyesho hilo. 
baadhi ya picha zinazoonesha huduma ya utoaji wa afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Tosamaganga , huduma hiyo ainayoendana manafumzo kwa wataalamu wa afya imeweza kuokoa maisha ya wanawake wajawazito pamoja na watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda.

Na  Mwandishi Maalum, New York

Tanzania  imeelezea kuridhishwa kwake na ushirikiano  uliopo baina ya  Serikali na  Taasisi Binafsi   katika  uboreshaji na utoaji wa huduma  za afya  zikiwamo zinazomlenga mama na mtoto. Na hivyo kuchangia katika upiguzaji wa vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Kauli hiyo imetolewa  siku ya  jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako  Manongi, wakati wa   uzinduzi wa onyesho  kwa njia ya picha kuhusu huduma  za afya zinazotolewa na   Taasisi isiyo ya kiserikali  ya  Doctors with Africa CUAMM inayofanya shughuli za   utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto katika Hospitali  ya Tosamaganga,  Mkoani  Iringa.

Picha hizo zinaonyeshwa katika  corridor za  Umoja wa Mataifa, sambamba na  mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake ( CSW) unaofanyika hapa Makao makuu ya Umoja wa Mataifa,  mkutano unaojadili masuala mbalimbali yanayomhusu mwanamke na mtoto wa kike, kuanzia elimu, fursa na haki sawa,  huduma bora za afya,  uwezeshwaji , haki za mwanamke na mtoto wa kike pamoja na changamoto zinazo wakabili.

Balozi Manongi amesema  ni kwa kushirikiana ndipo  nchi kama  Tanzania  inaweza  kuongeza kasi ya kuwafikishia huduma za afya wananchi wengi, na kuwa  uwepo wa Taasisi kama  ya  Doctors with Africa CUAMM na  mchango wake katika utoaji wa huduma za afya huko  Tosamaganga na maeneo mengine ni kielelezo  sahihi cha ushirikiano anaouzungumzia.

Akasema    mchango wa  Taasisi hiyo ni mfano wa kuigwa na  ndiyo maana Tanzania katika   maandalizi ya  malengo mapya  ya  maendeleo baada ya 2015 moja ya maeneo inayoyapigia chapuo ni pamoja na hilo la afya ya mama na mtoto pamoja na ushirikiano  miongoni mwa wadau mbalimbali.

“ Nyinyi ni kielelezo sahihi cha ubia na ushirikiano  tunaouhimiza. Asanteni sana kwa mchango wenu na asanteni  kwa kudhirisha kwamba inawezekana kufanya kazi kwa ushirikiano”. akasema Balozi.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Taasisi hiyo,  Bw. Andrea Atzori,  amesema Taasisi yake  ambayo  imekuwa nchini Tanzania  tangu mwaka 1968 imejielekeza   Zaidi katika utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya  vijijini  hususani kwa akina  mama wajawazito na watoto  wachanga wakiwamo wanaozaliwa kabla ya muda.

 Huduma nyingine   zinatolewa na taasisi hiyo  ni pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa afya,  huduma za uzazi salama kupitia mpango wao wa miaka mitano   walioupa  jina la “mama na mtoto kwanza”.

Aidha kwa mujibu wa Dkt. Andrea Atzori,  Taasisi hiyo inatarajiwa kupanua huduma zake katika maeneo mengine Zaidi  ya pembezoni kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma ya afya pale walipo.

Pamoja na  Tanzania,   Doctors with Africa CUAMM  iliyoanzishwa mwaka 1950 na makao yake yakiwa nchini Italia,pia inaendesha shughuli zake katika nchi za  Angola,  Ethiopia, Msumbiji,  Sudani ya Kusini, Uganda na  Sierra leone.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »