………………………………………………………………………………………………………………………
Na Anna Nkinda – Maelezo, Mafia
Wazazi na walezi wilayani Mafia
wametakiwa kutokubali kupokea mahari za watoto wao wakiwa wanafunzi
bali wawasimamie na kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kufika elimu ya
chuo kikuu.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akiongea na wanafunzi pamoja na wazazi wa shule ya Sekondari Bweni
iliyopo kata ya Kanga wilaya ya Mafia mkoani Pwani.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) alisema baadhi ya wazazi wanapokea mahari za watoto wao
na kuwaozesha wakiwa na umri mdogo jambo ambalo huwafanya kukatisha
masomo yao na wanawanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.
“Mtoto akisoma atakuwa na maisha mazuri hapo baadaye ataweza
kufanya kazi za kitaalamu za kuajiriwa au kujiajiri yeye mwenyewe,
kujikomboa na umaskini, kuwasaidia wazazi wake, ataepukana na mimba za
utotoni na kujiepusha na maradhi yanayotokana na ngono zembe kwani
elimu ni msingi wa kila kitu”.
Wanawake wenzangu mtoto wako wa kike akiwa mwali usikubali
kumuweka ndani ili asubiri mwanaume wa kumuoa na ukisikia mmeo kapokea
mahari ili binti huyo aolewe katoe taarifa sehemu inayohusika ili sheria
iweze kuchukua mkondo wake”, alisisitiza Mama Kikwete.
Kwa upande wa wanafunzi aliwaasa kujiepusha na kitendo cha
kujiingiza katika mapenzi wakiwa na umri mdogo bali wasome kwa bidhii ,
wawe na nidhamu kwa walimu wao na kuwa na malengo katika maisha yao kwa
kufanya hivyo watatimiza ndoto zao.
Alisema, “Wanangu someni kwa bidii msitake utajiri wa haraka,
watoto wa kiume mnaacha kwenda shule, mnakatisha masomo na kukimbilia
kuvua samaki kwa kudhani kuwa mtapata maendeleo kumbukeni elimu ni
urithi usioweza kutoweka katika maisha yenu”,.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwahimiza wazazi kwenda
Hospitali kupima ugonjwa wa saratani za shingo ya kizazi, matiti na tezi
dume ambazo zikigundulika katika hatua ya awali mgonjwa anaweza
kutibiwa na kupona kabisa.
Kuhusu utunzaji wa ardhi Mama Kikwete alisema wilaya hiyo
imejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba inayowavutia watu wengi na
kuwasihi wananchi kutoiuza kiholela bali waitunze, kama kuna
wawekezaji utaratibu maalum ufuatwe.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Ndekilo aliwahimiza
wananchi hao kuona umuhimu wa kuwarithisha watoto wao elimu ambayo ni
ufunguo wa maisha na siyo mali kama uvuvi, ng’ombe na mashamba.
Eng. Ndekilo alisema atakuwa mkali kwa mtu yoyote atakayekatisha
elimu ya mtoto wake na katika suala la mtoto kuacha shule baada ya
kupewa ujauzito mahakama ndiyo itakayotoa maamuzi na siyo wazazi
kumalizana wenyewe kwa wenyewe.
Akisoma taarifa ya shule Mwalimu mkuu Mohamed Msossow alisema
shule hiyo ilifunguliwa mwaka 2007 ikiwa na walimu wanne na wanafunzi
199 kati ya hao wavulana walikuwa 147 na wasichana 52 . Hivi sasa kuna
walimu 20 na wanafunzi 131 kati ya hao wavulana 61 wasichana 70 na
walimu 20.
Aliyataja mafanikio waliyo nayo ni walimu wa kutosha wa masomo
ya sanaa, vitabu vya kutosha vya masomo ya sayansi na sanaa kwa uwiano
wa mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja, madarasa ya kutosha, ushirikiano
mzuri na jamii inayowazunguka na matokeo mazuri ya kitaaluma katika
mitihani ya kidato cha pili na cha nne.
“Changamoto zinazotukabili ni upungufu wa walimu wa masomo ya
sayansi na hisabati, nyumba za walimu na vifaa vya maabara, kutokana na
mazingira ya mahali shule ilipo shule inahitajika kuwa na usafiri ili
kurahisisha walimu kufika wilayani”.
Idadi ndogo ya wanafunzi inayosababisha kupata mgao mdogo wa
fedha ya ruzuku kutoka Serikalini na kusababisha ugumu katika kuendesha
shughuli mbalimbali za shule, ukosefu wa umeme na uhaba wa vyanzo vya
maji”,alisema Mwalimu Msossow.
Mama Kikwete yuko wilayani humo kwa ziara ya kikazi ya siku
mbili na akiwa shuleni hapo aliwapatia wanafunzi zawadi ya shilingi
milioni moja.
Shule ya Sekondari Bweni imejengwa na Taasisi ya Maendeleo ya
Kisiwa cha Mafia (MIDEF) chini ya usimamizi wa Dkt. Ramadhan Dau ambaye
ni Mkurugenzi wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na
kuikabidhi kwa Serikali ambapo hivi sasa ni Shule ya Sekondari ya kata
ya Kanga.