Mkandarasi wa kampuni ya Kiure
Engineering iliyofanya Ukarabati Mkubwa katika kituo cha Jimolojia
Tanzania (TGC) cha Jijini Arusha, Oswald Modu ( wa tatu kulia)
akimkabithi funguo za vyumba mbalimbali vya kituo hicho, Mkurugenzi wa
Manunuzi Wizara ya Nishati na Madini Amon Makachayo (wa tatu kushoto).
Wengine wanaoshuhudia ni baadhi ya watumishi wa Wizara ya Nishati na
Madini na Wafanyakazi wa kampuni ya Kiure Engineering.
Mratibu wa Kituo cha Jimolojia
Tanzania (TGC) Mussa Shanyangi (wa pili kulia), akiwaonesha Mkurugenzi
wa Manunuzi Wizara ya Nishati na Madini Amon Makachayo (wa pili kushoto)
na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Habari na Teknolojia Francis
Fungameza namna mashine ya kukata mawe inavyofanya kazi.
Baadhi ya Wanafunzi katika kituo
cha Jimolojia Tanzania (TGC) waki polish mawe wakati wa mafunzo.
Wanafunzi hao wako katika mafunzo ya ukataji na unga’rishaji madini
katika kituo hicho.
Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu
wa Rasilimali Madini (SMMRP) Idrisa Yahya (kushoto) akimweleza jambo
Mkandarasi wa Kampuni ya Kiure Engineering Oswald Modu(wa tatu kulia)
wakati wa ukaguzi wa jingo la kituo hicho kabla ya makabidhiano rasmi
kufanywa.
Baadhi ya wanafunzi wa kituo cha
Jimolojia Tanzania (TGC) kilichopo Jijini Arusha. Wakiwa katika mafunzo
ya kunga’risha madini. Kituo hicho kitawezesha shughuli za Uongezaji
Thamani kufanyika chuoni hapo.
Sehemu ya Jengo la kituo cha
Jimolojia Tanzania TGC, inavyoonekana pichani baada ya Ukarabati Mkubwa
kufanywa na Kampuni ya Kiure Engineering. Jengo hilo limekabidhiwa rasmi
kwa kituo hicho mwishoni mwa wiki.
Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu
wa Rasilimali Madini (SMMRP) Idrisa Yahya (katikati) na ujumbe wa
Wizara na Mkandarasi wa Kampuni ya Kiure Engineering wakikagua mfumo wa
CCT katika kituo cha Jimolojia Tanzania. (TGC).
Baadhi ya Vinyango vilivyochongwa kwa madini yam awe katika kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC).
………………………………………………………………………………
Na Asteria Muhozya, Arusha
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa
ukarabati mkubwa wa kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) cha Jijini Arusha
ni mafanikio makubwa kwa Wizara ya Nishati na Madini hususan katika
tasnia ya Uongezaji Thamani Madini nchini kwani kitawezesha shughuli
hizo kufanyika nchini.
Hayo yamebainishwa na Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa
Rasilimali Madini (SMMRP) Idrisa Yahya mwishoni mwa wiki wakati wa
makabidhiano ya kituo hicho baada ya kukamilika kwa ukarabati mkubwa
uliofanywa na kampuni ya Kiure Engineering .
“Mkandarasi amejitahidi kufanya kazi katika muda tuliokubaliana
na kazi imefanyika kama ilivyotakiwa. Hivi sasa tutautaja kama mradi
uliokamilika”, alieleza Idrisa.
Aliongeza kuwa, mradi wa SMMRP utaendelea kukisaidia kituo hicho
ili kiweze kutimiza malengo yake na kuhakikisha kinatoa taaluma katika
masuala ya uongezaji thamani madini na hivyo kuwezesha sekta ya madini
kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Alisema kuwa, SMMRP imelenga katika kukiwezesha kituo hicho
kuwa bora katika mafunzo ya uongezaji thamani madini nchini kutokana na
umuhimu wa shughuli hizo kufanyika nchini badala ya madini hayo
kusafirishwa nje ya nchi yakiwa ghafi.
“Tumelenga katika kukiunganisha kituo hiki na vyuo vingine
duniani vinavyotoa taaluma katika masuala haya ili kupata uzoefu na
kubadilishana taaluma. Tunataka kituo hiki kifanye kazi iliyokusudiwa na
kisimame peke yake hivyo lazima kiweke mipango mizuri. Kwa upande wa
wizara ina budi kutenga bajeti ya kituo hiki kiendelee ili kutimiza
malengo tunayoyatarajia”, alisisitiza Idrisa.
Kwa upande wake Mratibu wa kituo hicho Musa Shanyangi alisema
kuwa, kituo hicho kinatarajia kuanza muhula mpya wa masomo ifikapo mwezi
Juni mwaka huu katika fani za ukataji madini, masuala ya jimolojia,
mafunzo ya usanifu na utengenezaji wa mapambo ya vito.
“Hivi sasa tunao wanafunzi 15 wanawake wanaosoma fani ya kukata
na kung’arisha madini. Wanafunzi hawa walianza mafunzo tangu Novemba
2014 na wanasoma kwa ufadhili wa Serikali kwa kushirikiana na Chama cha
Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA)” alisema Shanyangi.
Aidha, Shanyangi aliishukuru Serikali kwa kutambua shughuli za
uongezaji thamani madini nchini kwani zitaongeza wigo wa ajira, kipato
cha mtu mmoja mmoja, kuwezesha ukuaji wa shughuli za kiuchumi kupitia
sekta hiyo ikiwemo pia kuchangia katika pato la taifa.
Shughuli za uimarishaji na uendelezaji wa kituo hicho
zinafanyika chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini
(SMMRP). Kituo kitakuwa na maabara ya utambuzi wa madini ya vito,
maktaba ya jimolojia na makumbusho ya madini ya vito.
EmoticonEmoticon