Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
iliketi jana Jumapili tarehe 08 Februari, 2015 katika kikao chake cha kawaida.
Pamoja na kujadili maandalizi ya Mkutano Mkuu wa kawaida utakaofanyika
Machi 14 na 15 mjini Singida, Kamati ilijadili na kuamua yafuatayo:-
1.
Zoezi la utoaji leseni
kwa vilabu litaanza kabla ya msimu wa ligi 2015/16. Vilabu vitatumiwa
fomu za maombi mapema iwezekanavyo ili viweke nyumba zao sawa na kuleta maombi.
Leseni za vilabu (club licence) ni agizo la CAF na FIFA katika
kuhakikisha vilabu vinaendeshwa kwa weredi. Baadhi ya maeneo
yanayoagaliwa katika utoaji wa leseni ni pamoja na kuwepo kwa Sekretarieti,
miundo mbinu ya mazoezi na mashindano, hadhi za kisheria (legal status)
mikataba ya ajira n.k.
2.
Kamati ya Utendaji
imeazimia kufanyika kwa mashindano ya Taifa Cup kwa upande wa wanaume.
Sekretarieti ya TFF imetakiwa kufanya juhudi ili mashindao hayo yaweze
kufanyika.
3.
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania limetoa pongezi kwa Shirika la Taifa la hifadhi ya jamii (NSSF)
kwa juhudi zake za kukuza soka la vijana kupitia mradi wake wa kuanzisha shule
ya soka (Academy) kwa ushirikiano na klabu ya Real Madrid ya Hispania.
Aidha Kamati ya Utendaji ya TFF imeipongeza Kampuni ya Symbion na klabu
ya Sunderland ya Uingereza kwa juhudi zao za kuchangia maendeleo ya soka la
vijana na mpira wa miguu kwa ujumla ikiwa ni kupitia mpango wa kujenga shule ya
soka (academy) uwezeshaji wa mashindano ya vijana chini ya miaka 13 (U-13)
yatakayofanyika mwezi April, 2015 mjini Mwanza na ujenzi wa miundo mbinu ya
soka na michezo kwa ujumla.
Kamati ya Utendaji imewaomba wadau wengine
kufuata mifano hiyo na kuchangia maendeleo ya soka kwani kazi hii inategemeana
ni kwa faida ya wadau mbali mbali.
4.
Kamati ya Utendaji
ilipokea mabadiliko ya uwakilishi wa Chama cha Soka la Wanawake nchini (TWFA)
yaliyotokana na kuondoka kwa Bi. Lina Kessy aliyekuwa Mwenyekiti wake.
Bi. Lina ameajiriwa kama Afisa michezo wa Umoja wa Afrika (AU) mjini
Addis Ababa, Ethiopia. Nafasi ya Mwenyekiti inachukuliwa na Bi. Rose
Kisiwa ambaye hapo kabla alikuwa Makamu Mwenyekiti wa TWFA ataendelea kuwa
Mwenyekiti mpaka hapo utakapokaa Mkutano Mkuu wa kawaida wa TWFA.
5.
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kuwepo kwa vitendo vya
vurugu na utovu wa nidhamu katika mashindano mbalimbali yanayoendelea nchini.
TFF inatoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu hususani viongozi wa
vilabu kutilia mkazo elimu ya kujitambua ili wachezaji wajue kuwa wao ni hazina
ya Taifa na kioo (taswira) cha jamii, hivyo waepuke vitendo vya utovu wa
nidhamu ndani na nje ya uwanja. Vitendo hivi si tu vinakwamisha
maendeleo, bali pia vinawadharirisha wao, mpira wa miguu na jamii kwa ujumla.
Kufuatia matukio ya hivi
karibuni na kuzingatia umuhimu wa kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa haraka
na weredi, Kamati ya Utendaji imeteua ya Kamati ya kuangalia na kusimamia
kanuni za uendeshaji Ligi. Kamati hiyo itaundwa na wajumbe kutoka Bodi ya Ligi,
Kurugenzi ya mashindano, Kamati ya mashindano na kamati ya waamuzi.
TFF
YATUMA SALAMU ZA PONGEZI KWA FIF
Rais
wa Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini –TFF Bw Jamal Malinzi ametuma salama za
pongezi kwa Rais Sidy Diallo wa Shirikisho la soka nchini Ivory Coast
(FIF) kwa kutwaa Ubingwa wa Mataifa Afrika.
Katika
salam zake Bw. Malinzi amesema mafanikio hayo ya kutwaa Ubingwa wa Afrika
yametokana na juhudi za Rais huyo pamoja na Kamati yake ya Utendaji.
Kwa
niaba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), familia ya mpira na
watanzania kwa ujumla wanawapa pongezi Shirikisho la mpira wa Miguu la Ivory
Coast kwa kutwaa Ubingwa huo wa Afrika kwa mara pili.
SALAMU
ZA RAMBIRAMBI
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini – TFF amepeleka salamu za rambirambi kwa
Rais Mohamed Gamal wa Chama cha mpira wa miguu nchnii Misri (EFA ),kufuatia
vifo vya mashabiki vilivyotokea mwishoni wa wiki katika mchezo
uliowakutanisha Zamalek na ENPPI.
Mashabiki
wapatao ishirini na moja (22) wameripotiwa kupoteza maisha katika vurugu
hizo zilizowahusisha mashabiki wa Zamalek na ENPPI na kupelekea Shirikisho la
Soka nchini Misri kuisimamisha michezo ya Ligi nchini humo.
Katika
salam zake, kwa niaba ya TFF, familia ya mpira wa miguu na watanzania Rais
Malinzi amewaomba wapenzi wa soka nchini Misri kuwa wavumilivu katika
kipindi hiki cha maombelezo ya vifo vya mashabiki hao.
TFF YAIPONGEZA CAF
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF) Bw Jamal Malinzi
amemtumia salamu za pongezi Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) Bw
Issa Hayatou kwa kufanikiwa kuandaa salama fainali za Mataifa Afika nchini Equatorial Guinea bila ya kuwepo kwa ugonjwa
wa Ebola.
Katika
salamu hizo kwenda kwa Bw Haytou na nakala yake kupitia Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) Bw Hicham El Amrani, Bw
Malinzi amesema kwa pamoja analipongeza Shirikisho hilo na wenyeji wa michuano
kwa kufanikiwa kuandaa mashindano hayo na kumalizika salama.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
EmoticonEmoticon