Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama
Salma Kikwete amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutokubali kuuza maeneo ya
ufukwe wa Bahari ya Hindi kwa kiasi kidogo cha fedha kwani thamani ya
maeneo hayo ni kubwa.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akiongea kwa
nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho
katika matawi ya Raha leo na Ufukoni yaliyopo katika kata ya Rahaleo
wilayani humo.
Alisema hivi sasa kuna wageni
wengi ambao wanaenda kwa wananchi na kununua maeneo ya ufukweni kwa bei
ya chini lakini kama wamiliki wa maeneo hayo watakuwa na subira
watayauza kwa bei kubwa kwa kipindi cha miaka michache ijayo.
“Baada ya miaka michache ijayo
mkoa wetu utakuwa tofauti kimaendeleo, Serikali inampango wa kujenga
mji wa kisasa katika eneo la Mitwero.
“Nawasihi hata kama mtu anashida
kiasi gani atafute njia nyingine ya kupata fedha lakini siyo kuuza eneo
la ufukweni kwa bei ndogo, kama kuna aliyebakiza eneo lake asiuze
kwani kimfaacho mtu ni chake”, alisisitiza Mama Kikwete .
Kuhusu elimu MNEC huyo aliwasihi
viongozi hao kusimamia elimu ya watoto wao na kuwahimiza waende shule
kwani wakiwa na elimu wataweza kufanya kazi za kitaalamu katika sekta
mbalimbali ikiwemo ya gesi inayopatikana mkoani humo.
Kwa upande wa wanawake aliwahimiza
kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika
uchaguzi mkuu ujao na hivyo kufika katika ngazi ya maamuzi pia kwa
kufanya hivyo hawatapoteza haki yao ya msingi ya kuchaguliwa.
Akiwasalimia viongozi hao Mkuu wa
wilaya ya Lindi Dkt. Nassoro Hamidi alisema shule za Sekondari
zimefunguliwa lakini wanafunzi walioripoti shuleni ni wachache na
kuwaomba kupita nyumba hadi nyumba kuwahamasisha wazazi wawapeleke
watoto wao shule kwani bila ya elimu hakuna maendeleo.
“Serikali ilitoa agizo kama
watoto hawana ada au nguo za shule waende hivyo hivyo kuanza masomo
mambo mengine yatafuata baadaye lakini hadi sasa bado idadi ya wanafunzi
walioripoti shuleni ni ndogo”, alisema Dkt. Hamidi.
Kuhusu wananchi kujitolea katika
ujenzi wa maabara aliwasihi viongozi kuwahimiza kushiriki katika ujenzi
na maabara hizo ziweze kukamilika kwa wakati ili watoto wajifunze
masomo ya sayansi kwa vitendo.
Mama Kikwete yupo wilayani humo
kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya
vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka
2010 . Hadi sasa ameshatembelea matawi 64 kati ya 82 yaliyopo wilayani
humo.
EmoticonEmoticon