Waziri
Mkuu Mh. Mizengo Pinda akiwapongeza wachezaji wa timu za Bunge la
Jamuhuri kwenye tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2015 katika
majengo ya Bunge hilo Mjini Dodoma.
Waziri
Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Peter
Pinda aliwapongeza wanamichezo wa Timu za Bunge la Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa kuliletea sifa kubwa Bunge hilo kwenye mashindano ya
michezo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Mh.
Pinda alitoa pongezi hizo katika Tafrija maalum ya kuukaribisha mwaka
mpya zilizofanyika katika majengo ya Bunge la Jamuhuri Mjini Dodoma
hafla iliyokwenda sambamba na kuwapongeza wanamichezo wa Bunge hilo
baada ya kushinda michezo tofauti katika mashindano ya Mabunge ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Mjini Arusha Tanzania.
Waziri
Mkuu Pinda alisema kwamba michezo inatoa nafasi kubwa ya ushirikiano
ambayo ni kielelezo cha msingi kinachozaa Viongozi bora wanaotokana na
sekta ya michezo.
Waziri
Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda
akiwa pamoja na Spika wa Bunge Mh. Anna Makinda na Baadhi ya Wabunge
wakifurahia vikombe mbali mbali vilivyoibuliwa na Timu za Bunge la
Jamuhuri katika Mashindano ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aliishauri
Kamati ya Uongozi wa Michezo ya Bunge hilo kufikiria umuhimu wa
kuwashirikisha wawakilishi wa wanamichezo wa mabunge wanachama kwenye
tafrija kama hizo kwa lengo la kusherehekea nao pamoja ili kudumisha
ushirikiano pamoja na ujirani mwema.
Alieleza
kwamba michezo ina nafasi pana ya kupunguza joto la kisiasa, hitilafu
au ugomvi unaotokea baina ya nchi na nchi na kupelekea watu wa pande
zinazohitilafiana kurejea kwenye ushirikiano na mafungamano baina yao.
Mh.
Pinda alifahamisha kwamba kwa kuwa mabunge mengi yana utaratibu mzuri
wa kuandaa mashindano ni vyema kwa waheshimiwa wabunge kuzitumia fursa
kama hizo katika kushiriki kwenye mazoezi na hatimae mashindano kwa
lengo la kudumisha afya zao.
Baadhi
ya Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wakiwa kwenye tafrija ya
kuupokea mwaka mpya wa 2015 iliyofanyika katika majengo ya Bunge Mjini
Dodoma sambamba na kuzipongeza Timu za Bunge hilo zilizoshinda kwenye
mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki.
Waziri
Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliwatakia mwaka
mwema wa 2015 Waheshimiwa wote wa Bunge la Jamuhuri hasa mwezi Oktoba
mwaka huu ambao kama wamefanya vyema majimboni mwao utawarejesha tena
kwenye wadhifa wao.
Alisema
kurejea kwa Wabunge hao kwa kiasi kikubwa kunaweza kuleta faraja kubwa
kwa vile tayari wameshazoeana kutokana na kushirikiana pamoja katika
vikao vya Bunge hilo kwa takriban miaka mitano.
Mapema
Mwenyekiti wa Bunge Sports Club Iddi Azan alisema ongezeko la michezo
mbali mbali kwenye mashindano ya Timu za Mabunge ya Afrika ya Mashariki
linatokana na azimio la Mabunge ya Jumuiya hiyo la kuzitaka Nchi
Wanachama kuongeza michezo mengine kwenye mashindano hayo.
Waziri
Mkuu akiwaongoza waheshimiwa wenzake kwenye mduara ulioporomoshwa na
bendi ya Utalii katika tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2015 Mjini
Dodoma.(Picha na – OMPR – ZNZ).
Mwenyekiti
Azan alisema mshindano ya Mabunge hayo yalikuwa yakishirikisha michezo
miwili tuu ile ya Kandanda na Pete ambapo kwa sasa ipo riadha, mbio za
vijiti, kuvuta kamba, kufukuza kuku ikiwemo pia ile ya watu wenye
mahitaji maalum { Walemavu }.
Mwenyekiti
huyo wa Bunge Sports Club alielezea faraja yake kutokana na ushiriki
mzuri wa wanamichezo wa Timu za Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania kwenye mashindano mbali mbali ya Mabunge na kuleta ushindi
katika michezo tofauti.
Katika
mashindano hayo ya mwaka 2014 ya Timu za Mabunge ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki yaliyoshirikisha wachezaji 150 Timu ya Mpira wa Pete Wanawake
ya Bunge la Tanzania ilitokea mshindi wa kwanza, Riadha wanawake
washindi wa kwanza, riadha wanaume washindi wa Tatu, mpira wa miguu
washindi wa Pili na kuvuta kamba Timu za wanawake na wanaume Tanzania
zimeshika nafasi ya kwanza.
EmoticonEmoticon