Watu
wawili wamefariki dunia baada ya kimbunga kupiga katika Kisiwa cha
Goziba na kusababisha baadhi ya mitumbwi kupinduka katika Ziwa
Victoria.
Kimbunga
hicho kilitokea juzi saa tano asubuhi wakati wakazi mbalimbali wakiwa
katika shughuli zao.Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Rembris Kipuyo alisema
jana kuwa, majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Kagera.
Alisema
kimbunga hicho hakikuwa cha kawaida kwa kuwa kiliharibu nyumba na zaidi
ya mitumbwi arobaini imepotea.Miongoni mwa walionusurika, Mariagoreth
Phares alisema tukio hilo lilikuwa kama muujiza kwa kuwa aliona kitu
kilichosogea kutoka angani.
Alisema
nyumba zilianza kung’olewa kwa upepo na watu kurushwa majini, huku
wengine wakipoteza fahamu.Alisema baadhi ya watu walikuwa wakijaribu
kujiokoa kwa kutambaa ili wasipigwe na vitu vilivyokuwa viking’olewa na
kurushwa na upepo.
Majeruhi mwingine Leah Lazaro alisema aliona kitu kilichokuwa kinachemsha maji kwa kasi ziwani kuelekea kwenye kisiwa hicho.
“Nilikuwa
mwaloni nikaona kitu kinachemsha maji kwa kasi nilikimbia na
kumkumbatia mtoto wangu ambaye aliniponyoka,” alisema Lazaro.
Kisiwa cha Goziba kipo umbali wa kilomita 80 kutoka Wilaya ya Muleba na kipo karibu zaidi na Mkoa wa Mwanza.
Wakazi
wa kisiwa hicho hupata mahitaji yao Mwanza. Kipuyo alisema baada ya
kamati ya maafa kutembelea eneo hilo, itatoa tathimini ya kiwango cha
hasara kilichotokea.
Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wakazi wa kisiwa hicho ambao wengi wao wamepoteza mali.