Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete akizungumza katika kikao cha ndani na wajumbe wa Tawi
la Nanyanje lililopo katika Kata ya Chikonji katika wilaya ya Lindi
Mjini tarehe 12.12.2014.
Mjumbe
wa NEC Taifa ya CCM na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwapungia
wananchi wa Kata ya Chikonji wakati alipofika kwenye Makao Makuu ya Kata
hiyo kwa ajili ya mkutano wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa serikali
za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini tarehe 14.12.2014.
Mamia
ya wananchi waliofurika katika mkutano wa kampeni ulifanyika katika
Kata ya Chikonji iliyoko katika Wilaya ya Lindi Mjini na kuhutubiwa na
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mama Salma Kikwete tarehe
12.12.2014.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mke wa Rais Mama Salma
Kikwete akijiandaa kupokea kadi kutoka kwa Ndugu Abdallah Mohammed
Kilimbalimba aliyekuwa mwanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF) ambaye
aliamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi wakati wa mkutano wa kampeni
huko Chikonji katika Wilaya ya Lindi Mjini tarehe 12.12.2014.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayewakilisha Wilaya ya Lindi
Mjini na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwahutubia mamia ya wananchi
wa Kata ya Chikonji kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa serikali za
mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini tarehe 14.12.2014.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akimchukua mtoto Subira kutoka kwa mama yake
ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja wakati wa mkutano wa
kampeni huko Chikonji taqrehe 12.12.2014.
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
akiwasili kwenye Tawi la Makonde lililoko kwenye Kata ya
Mingoyo katika Wilaya ya Lindi Mjini huku akipokewa kwa shangwe na
vifijo kwa ajili ya mkutano wa kampeni tawini hapo tarehe 12.12.2014.
Baadhi
ya akina mama wakishangilia kwa hisia kubwa wakati Mama Salma Kikwete
alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Mingoyo
uliofanyika katika Tawi la Makonde tarehe 12.12.2014.
Mke
wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Taifa Mama Salma
Kikwete akihutubia mkutano wa kampeni katika Tawi la Makonde lililoko
katika kata ya Mingoyo tarehe 12.12.2014.
PICHA NA JOHN LUKUWI
……………………………………………………………………………………..
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
13/12/2014 Wakazi wa wilaya ya
Lindi mjini wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule na kusoma
kwa bidii kwani Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imejenga shule za
kutosha katika kata zote za wilaya hiyo.
Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini
Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi
waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa
Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata za Chikonji na Mingoyo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema wakati ujenzi wa shule hizo unaanza
vyama vya upinzani walizidharau na waliziita za yeboyebu kwa lengo la
kuwakatisha tamaa lakini Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi
hawakukata tamaa na kuendelea na ujenzi.
“Zamani wanafunzi waliokuwa
wanajiunga na elimu ya Sekondari walikuwa wachache baada ya kukamilika
kwa ujenzi wa shule hizi hivi sasa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani wa
darasa la saba anajiunga na elimu ya Sekondari haya ndiyo maendeleo
yaliyoletwa na CCM”.
Ili uweze kuendelea ni lazima
ukutane na changamoto nasi katika shule hizi tulikutana na changamoto za
walimu na maabara, vyuo mbalimbali nchini viliweza kutoa walimu wengi
na kupunguza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa na miaka michache
ijayo watapatikana walimu wa kutosha wa masomo ya sayansi”, alisema Mama
Kikwete.
Aliendelea kusema wakati wa ujenzi
wa shule za Sekondari za Kata kulisahaulika ujenzi wa maabara kwa ajili
ya masomo ya sayansi, hivi sasa Serikali kwa kushirikiana na wananchi
wanamalizia kazi ya ujenzi wa maabara katika shule hizo na hivyo
kuwafanya watoto kusoma masomo ya sayansi kwa fasaha zaidi.
MNEC huyo pia aliwataka wananchi
hao kuchagua viongozi wanaofaa kwani uchaguzi ni kwa ajili ya
kutengeneza maisha yao kwa kipindi cha miaka mitano hivyo basi wasiweke
rehani maisha yao kwa kufuata mkumbo na kuchagua viongozi wasiofaa.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa
wa Lindi Adelina Gefi alisema katika uchaguzi wa Serikali za mitaa,
vijiji na vitongoji chama hicho kitapata ushindi wa kishindo kwani hadi
hivi sasa ndani ya mkoa huo wagombea katika vitongoji 600, vijiji 80 na
mitaa saba wamepita bila kupingwa.
Gefi alisema CCM inaleta maendeleo
na upinzani unachelewesha hivyo basi siku ya uchaguzi ikifika wananchi
wajitokeze kwa wingi na kuwachagua wagombea wa chama hicho ili
wawaletee maendeleo.
Katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kata ya Chikonji mwanachama mmoja aliyejulikana kwa jina la
Abdallah Mohammed Kilimbalimba kutoka Chama cha Wananchi (CUF)
alijiunga na Chama Cha Mapinduzi.
Mama Kikwete yupo wilayani humo
kwa ajili ya kushiriki kwenye kampeni na kuwanadi wagombea wa chama
hicho wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa
viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa
kufanyika kesho nchini.
EmoticonEmoticon