Kiongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (Watatu kushoto) akimsikiliza kwa makini
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) mara
walipowasili katika bandari hiyo kujionea shughuli mbalimbali za
maendeleo bandari hapo.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto)
akiwaongoza wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango kujionea moja ya meli za kigeni zinazotia nanga katika
bandari hiyo. Meli hiyo ni MV Rwegura kutoka nchini Burundi.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) akitoa
ufafanuzi juu ya namna bandari yake inavyohudumia meli kutoka nchi
jirani. Wanaomsikiliza ni Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiongozwa na Bibi Florence Mwanri
(Kushoto aliyevaa fulana nyeusi).
Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ikiwa katika picha ya pamoja katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato nchini
(TRA) zilizopo kwenye Bandari ya Kasanga.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto)
akimfafanualia jambo Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia)
wakati akimkabidhi taarifa ya maendeleo ya bandari hiyo.
…………………………………………………………………….
Na Saidi Mkabakuli, Sumbawanga
Serikali imeazimia kuanza
kuiboresha bandari ya kimkakati ya Kasanga inayohudumia nchi za Burundi,
Rwanda na Kongo iliyopo katika Ziwa Tanganyika, mkoani Rukwa.
Ahadi hiyo imetolewa na Kiongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua
maendeleo ya miundombinu katika Bandari ya Kasanga.
Bibi Mwanri alisema kuwa serikali
kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imepanga kuboresha bandari zote ili
kuwa malango kuu la biashara kwa soko la ndani na kwa nchi jirani ili
kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kwa ufanisi.
“Tumedhamiria kuendelea kuboresha
miundombinu ya bandari hususan miradi iliyoibuliwa katika Programu ya
Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo Bandari ya Kasanga ili kuweza kukidhi
mahitaji ya utoaji wa huduma katika eneo hili,” alisema.
Bibi Mwanri aliongeza kuwa
serikali pia imejipanga kuendelea kuboresha miundombinu na ununuzi wa
vifaa mbalimbali vya kuhudumia shehena katika bandari za Dar es Salaam,
Tanga, Mtwara, Kasanga na Kigoma na kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa
bandari mpya za Mwambani (Tanga), Mbegani (Bagamoyo) na Bandari Kavu ya
Kisarawe.
Akizungumza na ugeni huo,
Msimamizi Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa
alisema kuwa Bandari hiyo ina fursa nyingi katika kuhudumia shehena na
abiria wanaopitia bandarini hapo.
“Bandari yetu ina fursa kubwa za
kibiashara kwani tuna wateja wengi kutoka ndani na nje ya nchi
wanaotumia bandari yetu kupitishia bidhaa zao, pamoja na abiria
wanaosafiri kwenda nje na ndani ya Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo
kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imedhamiria kuboresha mazingira
yatakayowezesha sekta binafsi kuwekeza katika kujenga miuondombinu na
kuboresha usafirishaji wa mizigo katika bandari zote nchini.
Pia, Mpango huo unaweka bayana kuendeleza na ukarabati na ununuzi wa vyombo vya usafiri na usafirishaji katika maziwa.
EmoticonEmoticon