Na Baraka Mbolembole,
Kiungo wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jonas Mkude
amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu yake ya
Simba. Mkude, 21 ni moja ya matinda ya kikosi cha pili cha mabingwa hao
mara 19 wa kihistoria wa Tanzania Bara, amepatiwa gari aina ya Toyota GX
115, huku pia kiwango chake cha mshahara kikipanda.
Mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo ambaye atafikisha miaka 22 Disemba
3, ni mchezaji muhimu katika timu hiyo na alikuwa akihusishwa na mpango
wa kusajiliwa na klabu ya Yanga SC na Azam FC lakini kitendo cha kusaini
klabu iliyomlea ni kama kumaliza mbio za timu hizo ambazo zilionesha
nia ya kumuhitaji kiungo huyo wa ulinzi.
Habari za ndani kutoka klabu ya Simba zinadai kuwa kiungo raia wa
Burundi, Pierre Kwizera anaweza kutemwa klabuni hapo baada ya kuonyesha
kiwango cha chini huku akishindwa kuendana na uchezaji wa timu hiyo.
Kwizera ni mzuri katika kupanga mashambulizi pekee, wakati Mkude anaweza
kukaba na kuichezesha timu. Wote wawili hucheza kama viungo wa chini na
ili kuendelea kuijenga timu hiyo, Simba imeona ni bora kumuongezea
mshahara, na kumpatia kile alichokuwa akihitaji Mkude kwa kuwa
wataendelea kupata huduma nzuri..
EmoticonEmoticon