RAIS AFANYA MAGEUZI: MKUU WA MKOA NA WA WILAYA TANGA WAHAMISHWA.

November 06, 2014
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewaapisha wakuu wa mikoa baada ya kufanya mabadiliko kwa wakuu wapya wanne wa Mikoa, na kuwahamisha wengine sita.
Halima Omari Dendego
Wakuu wapya wa Mikoa ni Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.


Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa
Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma,  Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.

Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.

Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.

Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi.

Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »