Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI
Genilson Santana Santos ‘Jaja’ amejiondoa Yanga SC akiwa likizo nchini
mwao, Brazil na sasa nafasi yake itazibwa na kiungo mkabaji, Emerson
Oliveira Neves Roque, BIN ZUBEIRY imeipata hiyo.
Jaja
amesema ana matatizo ya kifamilia yanayomzuia kurejea Tanzania kufanya
kazi- lakini BIN ZUBEIRY inafahamu mshambuliaji huyo ameshindwa kumudu
presha ya mashabiki wa klabu ya Jangwani.
Wapenzi wa Yanga SC hawajaridhishwa na uwezo wa Jaja, aliyeichezea klabu hiyo mechi 11 na kuifungia mabao sita.
Kocha
Maximo ambaye yuko likizo Brazil pamoja na Msaidizi wake, Leonardo
Leiva na kiungo Andrey Coutinho, amewatumia taarifa Yanga SC kwamba Jaja
hatakuja, badala yake anakuja kiungo mkabaji Emerson.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 mzaliwa wa Rio de Janeiro, anakuja Yanga SC akitokea klabu ya
Bonsucesso ya mjini humo, ambayo imewahi kucheza Ligi ya Serie B mara mbili, ingawa kwa sasa inacheza ligi ya jimbo la Rio.
Mchezaji
huyo anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Jumanne kwa ajili ya kufanyiwa
majaribio na akifuzu atafanyiwa vipimo vya afya, kabla ya kusajiliwa.
Wazi mchezaji huyo ana nafasi ya kusajiliwa Yanga SC kwa kuwa analetwa
na kocha Maximo.
Jaja
alijiunga na Yanga SC msimu huu, lakini hakuwahi kuwavutia wapenzi wa
klabu hiyo, ingawa atakumbukwa kwa mabao yake mawili aliyofunga wakati
Yanga SC ikiifunga Azam FC 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii Septemba
14, mwaka huu.
Genilson Santana Santos 'Jaja' anaondoka Yanga SC baada ya kuichezea mechi 11 na kuifungia mabao sita |
Jaja atakumbukwa kwa mabao yake mawili aliyofunga katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC, mechi ya Ngao ya Jamii |
EmoticonEmoticon