IFM YAANZA VEMA MASHINDANO YA SHIMUTA ,YAIBAMIZA TANGA CEMENT MABAO 2-1.

November 22, 2014

MKUU WA WILAYA YA MUHEZA,SUBIRA MGALU AKIKAGUA TIMU YA IFM LEO

 TIMU ya Kiwanda Cha Cement Mkoani Tanga(Tanga Cement) leo imeanza vibaya mashindano ya Shimuta baada ya kujikuta wakitandikwa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha Dar es Salaam (IFM) katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa uwanja wa CCM Mkwakwani.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani wa hali ya juu ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko IFM walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Yasin Mkumbo ambaye alitumia uzembe wa mabeki wa Tanga Cement na kupachika wavuni bao hilo.
 
MKUU WA WILAYA YA MUHEZA,SUBIRA MGALU AKIIKAGUA TIMU YA TANGA CEMENT LEO
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kila timu iliingia uwanjani hapo zikiwa na lengo la kuhakikisha zinapata matokeo mazuri kwenye ngwe hiyo ya lala salama iliyokuwa ikichezwa na mwamuzi Ibrahimu Kidiwa.

Wakionekana kujipanga baada ya kuwa nyuma bao 1-0,Tanga Cement waliweza kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa IFM na kufanikiwa kuandika bao la kufutia machozi kupitia mchezaji wake Daud Izack.

Baada ya bao hilo Tanga Cement waliweza kujipanga na kuendeleza mashambulizi mfululizo langoni mwa IFM bila mafanikio yoyote kutokana na wachezaji wake kupata mipira na kuipiga nje ya lango la wapinzani wao.


Kutokana na shambulio hilo,IFM waliweza kucharuka na kupeleka mashambulizi langoni mwa Tanga Cement na kufanikiwa kuandika bao la pili ambalo lilifungwa na Steven Shekiondo ambaye aliamsha shangwe na nderemo kwa mashabiki wao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »