UKATA WAIZIKWAMISHA TIMU ZA KIKAPU TANGA KUSHIRIKI MASHINDANO YA TAIFA CUP MWAKA HUU

November 23, 2014
TIMU ya Mkoa wa Tanga ya Mpira wa Kikapu imeshindwa kwenda kushiriki mashindano ya Taifa Cup ya mchezo huo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho mjini Dodoma kutokana na kukosa fedha za kuipelekea timu kwenye mashindano hayo.

Akizungumza na Tanga Raha Blog,Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Tanga,(TRBA)Hamisi Jaffary alisema kuwa kutokana na fedha ambazo timu hiyo ilikuwa ikiziitaji kwa ajili ya ushiriki wao kwenye michuano hiyo kiasi cha milioni sita kushindwa kupatikana wakashindwa kwenda kushiriki licha ya kufanya maandalizi.

Jaffary alisema kuwa licha ya kuwepo kwa sababu hiyo lakini pia wachezaji wengi wanaoichezea timu hiyo ni wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari mkoani hapa na walishindwa kupewa ruhusa kutokana na maandalizi yao ya Mashindano ya Bandari yatakayochezwa hivi karibuni hapa nchini.

Alisema kuwa chama hicho kiliwaombea ruhusa wachezaji hao lakini walishindwa kupewa ridhaa ya kuwatumia jambo ambalo pia lilionekana kuleta ugumu mkubwa kwao licha ya kutokuwa na fedha za kushiriki mashindano hayo.

    “Sisi kama chama tuliomba ruhusa kwa mwajiri wao kuhusu kuwatumia wachezaji hao lakini tuliambiwa kuwa wachezaji hao wanajiandaa na mashindano ya Bandari hivyo itakuwa ni vigumu kuwapata “Alisema Hamisi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mipra wa Kikapu mkoani hapa.

Hata hivyo,Mwenyekiti huyo aliwataka wadau wa michezo mkoani hapa kuendelea kukiunga mkono chama hicho kwa kukisapoti ili kiweza kufikia malengo yake ambayo kimejiwekea.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »