Naibu
Waziri wa Fedha –Sera, Mhe. Mwigulu Nchemba akifungua mafunzo ya wiki
tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika
kaya mwaka 2014/15.
Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera akiwakaribisha washiriki wa
mafunzo ya wiki 3 ya utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya
mwaka 2014/15 mkoani Morogoro.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumzia
umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya
wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya
nchini mwaka 2014/15.
Naibu
Waziri wa Fedha –Sera, Mhe. Mwigulu Nchemba akisalimiana na Mkuu wa
mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki
tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika
kaya mwaka 2014/15 mkoani Morogoro.
Washiriki
wa mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali
ya umasikini katika kaya nchini mwaka 2014/15 yanayofanyika mkoani
Morogoro wakifuatilia masuala mbalimbali .
WANANCHI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWA WATAALAM WA UTAFITI WA HALI YA UMASIKINI WA KAYA TANZANIA.
Na. Mwandishi wetu – Morogoro.
19/9/2014.
Serikali
imewataka wananchi na viongozi wa maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha
kuwa wanatoa ushirikiano kwa wadadisi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu
watakaoendesha zoezi la utafiti wa ukusanyaji wa takwimu za kufuatilia
hali ya umasikini katika kaya kwa mwaka 2014/2015, utaokaofanyika
kuanzia Oktoba mwaka huu.
Kauli
hiyo imetolewa jana mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Fedha –Sera,
Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akifungua mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi,
Wasimamizi na wadadisi watakaoendesha utafiti huo kutoka Tanzania Bara
na Zanzibar.
Amesema
serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa upande wa Bara na ile
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar imeamua kufanya utafiti huo ili
kupata takwimu bora na sahihi zitakazoiwezesha kujitathmini na kupima
juhudi zake katika kuwaletea wananchi maendeleo, kukuza uchumi na
kupunguza umasikini wa kipato.
“Kufanyika
kwa utafiti huu kutatuwezesha kufahamu namna na sababu zinazofanya kaya
kuendelea kubakia kwenye umasikini , baadhi ya kaya kutoka kwenye
umasikini na nyingine kuingia kwenye umasikini” Amesema.
Ameongeza
kuwa kukamilika kwa utafiti huo kutaiwezesha serikali kuelewa kwa kina
changamoto zinazoikabili katika utekelezaji wa Sera, mikakati na
programu mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.
Mhe.
Mwigulu amefafanua kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha Ofisi ya Taifa
ya Takwimu kwa kuijengea uwezo ili iweze kukamilisha tafiti mbalimbali
zinazoendelea kufanyika nchini kwa kufikisha matokeo ya tafiti hizo
katika ngazi zote za utawala.
“Nia
yetu ni kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo ya wananchi inapangwa kwa
kutumia takwimu rasmi, kwa upande wetu serikali takwimu rasmi ni
masikio na macho katika utendaji wa kazi za kilia siku” Amesisitiza Mh.
Mwigulu.
Aidha,
amewataka wakufunzi, wasimamizi na wadadisi watakaoendesha zoezi hilo
walio kwenye mafunzo hayo kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote
watakayopita kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo kwa taifa na kusisitiza
kuwa serikali haitawavumilia wadadisi watakaokiuka maadili katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina
Chuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa
washiriki wa mafunzo hayo watakaofaulu wataruhusiwa kushiriki katika
utafiti huo.
Amesema
kuwa utafiti huo hufanyika kila baada ya miaka 2 kwa kuzipitia kaya
binafsi ambazo huhojiwa kwa vipindi tofafuti ili kupata ufahamu wa namna
ambavyo kaya zinaingia na kutoka kwenye hali ya umasikini wa kipato na
sababu zinazochangia hali hiyo.
Ameeleza
kuwa kwa mwaka huu utafiti huo utakuwa wa nne kufanyika hapa nchini
ukitanguliwa na zile zilizofanyika mwaka 2008/09, 2010/11 na 2012/13.
Amefafanua
kuwa madodoso ya utafiti huo yatafuatilia na kukusanya taarifa muhimu
za sekta nyingine muhimu ambazo zinaweza kuchambuliwa kwa kuhusishwa
na hali ya umasikini zikiwemo kilimo, uvuvi, mifugo, Afya, Ajira na
Upatikanaji wa huduma za maji, umeme, afya na elimu.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera awali akizungumza
wakati wa kuwakaribisha washiriki wa mafunzo hayo mkoani Morogoro
amesema kuwa bila takwimu sahihi hakuna mipango ya maendeleo inayoweza
kufanyika.
Amesema kuwa kukamilika kwa utafiti huo kutatoa picha halisi ya nini kifanyike katika kuwaletea maendeleo wananchi.
EmoticonEmoticon