Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
HATIMAYE
michuano mikubwa kabisa ya soka nchini, ijulikanayo kama Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara inarejea tena kwa mara ya 51 tangu ilipoanzishwa
mwaka 1965 kwa wigo finyu na hali dunia kabisa, ikishirikisha klabu za
Dar es Salaam pekee.
Naam,
msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), unatarajiwa kuanza Jumamosi ya
leo, timu 14 zikijitupa dimbani kuwania pointi za mwanzoni, katika mbio
za kusaka ubingwa wa ligi, unaoshikiliwa na Wana Jangwani, Yanga SC.
Historia
ya ligi hiyo inaanzia mwaka 1929 ilipoanzishwa kifukara, tu kwa sababu
ya mapenzi ya watu na soka wakaamua kuungana na kuanzisha michuano ya
kutafuta bingwa, ingawa ni timu za Dar es Salaam pekee zilizokuwa
zikishiriki wakati huo.
Kufika
mwaka 1965, ilianzishwa michuano ya Klabu Bingwa Tanzania, ambayo
ilikuwa inaanzia ngazi ya Wilaya, ikichezwa kwa mtindo wa mtoano, ingawa
pia katika miaka miwili ya mwanzoni, timu za Dar es Salaama pekee ndizo
zilizoshiriki.
Katika
mfumo huo, bingwa wa kwanza ilikuwa ni klabu ya Sunderland ambayo hivi
sasa inajulikana kama Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo ilifanikiwa
kutetea ubingwa wake msimu uliofuata, kabla ya kuutema kwa Cosmopolitan
ya Dar es Salaam pia mwaka 1967.
Lakini
wakati wote huo, bado Tanzania ilikuwa haijawa mwanachama wa Shirikisho
la Soka la Kimataifa (FIFA), hivyo Sunderland hawakuwahi kucheza
michuano ya Afrika. Cosmo ingekuwa ya kwanza kucheza Klabu Bingwa Afrika
mwaka 1968 kama isingejitoa, lakini kwa kujitoa kwao, Yanga ilifungua
historia ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika
mwaka 1969, baada ya kutwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya kwanza mwaka
1968, kabla ya kuutetea mara nne mfululizo, katika miaka ya 1969, 1970,
1971 na 1972. Baada ya hapo, Sunderland ikiwa tayari imebadili jina na
kuitwa Simba kurejesha taji lake mwaka 1973.
Simba
ilishindwa kuutetea ubingwa wake msimu uliofuata mwaka 1974 baada ya
kupokonywa na Yanga katika fainali ya kihistoria iliyofanyika Uwanja wa
Nyamagana mjini Mwanza kwa kuchapwa mabao 2-1.
Mwaka
1975 Yanga iliutema ubingwa huo kwa Mseto SC ya Morogoro, iliyoweka
historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam kutwaa
ubingwa wa nchi.
Lakini
Mseto ilishindwa kuteteqa taji hilo, ikapokonywa na Simba msimu
uliofuata- na Wekundu wa Msimbazi walifanikiwa kutetea ubingwa huo kwa
miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.
Siri
ya kutawala kwa Simba kwenye ligi hiyo kwa miaka yote hiyo ni kuyumba
kwa Yanga baada ya kukumbwa na mgogoro mkubwa 1976, uliosababisha
kukimbiwa na wachezaji wote nyota, hivyo kuanza upya kabisa kuunda
timu.
Ni
ndani ya kipindi hicho Simba iliweza kulipa kisasi cha kuchapwa mabao
5-0 na Yanga mwaka 1968, wakati nayo ilipowatandika watani wao hao wa
jadi 6-0 mwaka 1977.
Juni
1, mwaka 1968 Yanga iliigaragaza Simba 5-0, mabao yake yakitiwa kimiani
na Maulid Dilunga (sasa marehemu) katika dakika za 18 kwa njia ya
penalti na 43, wakati mengine yalitiwa kimiani na Salehe Zimbwe dakika
ya 54 na 89 kabla ya Kitwana Manara kupachika la kuhitimisha karamu ya
mabao dakika ya 86.
Julai
19, mwaka 1977 Simba nayo ililipa kisasi kwa kuibugiza Yanga mabao 6-0,
wafungaji wakiwa ni Abdallah 'King' Kibadeni aliyetikisa nyavu mara
tatu katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mengine yalifungwa na Jumanne
Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73 na Selemani Sanga wa Yanga
alijifunga dakika ya 20.
Kufika
mwaka 1981, tayari Yanga ilikuwa imara tena na kufanikiwa kutwaa
ubingwa wa Tanzania Bara ingawa msimu uliofuata iliutema kwa Pan
African.
Kuanzia
mwaka 1982, mfumo wa Ligi ya Tanzania ulibadilishwa na kukawa na ligi
tatu, kwanza ni Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Ligi Daraja la
Kwanza visiwani Zanzibar na Ligi Kuu ya Muungano.
Yaani
baada ya kupatikana washindi wawili wa juu wa kila ligi, Bara na
Visiwani, walikutana kwenye Ligi Kuu ya Muungano, kutafuta bingwa wa
Tanzania na washindi wake.
Wakati huo, bingwa wa Ligi ya Muungano alikwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili alicheza Kombe la Washindi.
Baadaye timu ziliongezwa na kuwa tatu kila upande katika Ligi ya Muungano.
Mwaka
1983, Yanga ilirejesha taji hilo kwenye himaya yake, ingawa msimu
uliofuata ililitema tena kwa Simba. Kwa ujumla muongo mzima wa 1980,
taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara lilikuwa la kukoponyana, kwani Simba
nayo mwaka 1985 ilipokonywa taji hilo na Yanga, ambayo nayo ililitema
kwa timu mpya katika Ligi Kuu msimu wa 1986, Tukuyu Stars ya Mbeya.
Tukuyu
nayo iliwarejeshea Yanga taji lao mwaka 1987, wakati mwaka 1988 Wagosi
wa Kaya, Coastal Union ya Tanga ilijiingiza katika orodha ya timu
zilizowahi kutwaa taji hilo. Mwaka 1989, Yanga ilifunga orodha ya
mabingwa ya mabingwa wa muongo huo kwa kutwaa tena ubingwa wa Bara.
Simba iliibuka mwaka 1990 na kutwaa ubingwa huo, ikitoka kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita.
Kupokonyana taji kuliendelea hata kwenye muongo wa 1990, kwani Simba iliutema ubingwa huo kwa Yanga mwaka 1991.
Yanga
iliutetea ubingwa huo mara mbili mfululizo katika miaka ya 1992 na
1993, kabla ya kupokonywa na Simba mwaka 1994. Simba ilifanikiwa
kuutetea mara moja 1995.
Mwaka
1996 ndipo Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilipozaliwa rasmi chini ya
udhamini wa Bia ya Safari Lager, bia inayozalishwa na Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL) na ikijulikana kama Safari Lager Premier League, Yanga
ndiyo iliyokuwa bingwa wake wa kwanza. Yanga iliutetea ubingwa huo kwa
miaka miwili mfululizo 1997 na 1998. Mwaka 1999, Yanga ikiwa tayari
imetwaa ubingwa kwa matokeo ya uwanjani, aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa
Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani
Kapuya, alitengua matokeo hayo kwa kuiongezea Mtibwa Sugar pointi za
mezani, hivyo kuipiku Yanga. Hatimaye Mtibwa ilipata ubingwa wa mezani.
Mtibwa
ilifanikiwa kutetea ubingwa mwaka 2000, kabla ya kupokonywa na Simba
msimu uliofuata, ingawa Yanga iliibuka mwaka 2002 na kuutwaa tena
ubingwa huo.
Mwaka
2003 Simba iliyokuwa kali zaidi ilifanikiwa kuutwaa tena ubingwa huo na
kuutetea mwaka 2004 kabla ya kupokonywa na Yanga 2005 ambao waliutetea
2006. Mwaka 2007, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya mabadiliko
ya kalenda yake, ikitaka Ligi yake iendane na ligi za Ulaya, hivyo
ikaamua kuchezesha ligi ndogo ya mpito kumpata bingwa na mwakilishi wa
Kombe la Shirikisho, kabla ya Ligi Kuu kuanza rasmi Agosti.
Simba
iliibuka bingwa wa ligi hiyo, baada ya kuifunga Yanga kwenye fainali
kwa mikwaju ya penalti 5-4, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kufuatia sare ya
1-1.
Lakini
msimu uliofuata ikiwa chini ya Profesa wa Kiserbia, Dusan Savo Kondic,
Yanga ilifanikiwa kuurejesha ubingwa wake msimu wa 2008 na kutetea msimu
uliofuata ikiwa chini ya kocha huyo, ambaye hata hivyo msimu uliopita
alitupiwa virago katia mzunguko wa kwanza tu wa ligi na nafasi yake
kuchukuliwa na Mserbia mwenzake, Kostadin Bozidar Papic, ambaye
alishindwa kubakisha taji Jangwani, baada ya Simba kuchukua kwa
kishindo.
Simba
ilishinda mechi zote ikiwemo mbili dhidi ya watani wa jadi, Yanga na
kutoa sare mbili tu dhidi ya Kagera Sugar Bukoba na African Lyon Dar es
Salaam, hivyo kutwaa ubingwa kwa mbwembwe za aina yake na kufanikiwa
kuutetea 2010.
Mwaka
2011 taji lilikwenda Jangwani yalipo maskani ya Yanga SC, kabla ya 2012
kuhamia Msimbazi kwa Simba SC. Mwaka 2013 Yanga walirudisha taji lao
na Mei mwaka huu, Azam FC iliweka historia ya kutwaa kwa mara ya kwanza
ubingwa wa ligi hiyo.
Wakati
Ligi Kuu ikizipoteza timu za Ashanti United, JKT Oljoro na Rhino
Rangers zilizoterenka daraja msimu uliopita, msimu huu zimeibuka timu
nyingine ambazo ni Polisi ya Morogoro, Stand United ya Shinyanga na
Ndanda FC ya Mtwara.
Polisi
imewahi kucheza Ligi Kuu mara kadhaa na kuteremka kuanzia muongo
uliopita, wakati Ndanda na Stand zinapanda kwa mara ya kwanza.
Pazia
la kuashiria kufunguliwa kwa msimu uliopita lilipenuliwa rasmi kwa
mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga SC na Azam Jumapili iliyopita
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga SC walishinda 3-0.
Mechi
za ufunguzi leo zinatarajiwa kuwa kati ya mabingwa watetezi, Azam FC na
Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Yanga SC waliomaliza
nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro,
washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa
Sokoine, Mbeya.
Stand
United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage,
Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini,
Mlandizi mkoani Pwani, wakati washindi wa nne, Simba SC wataanza na
Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kilio
kikubwa cha wapenzi wa soka nchini ni kuhusu waamuzi, hawa wamekuwa
wakilalamikiwa sana kwa kuharibu ladha ya ligi, kutokana na kuzibeba
baaadhi ya timu.
Kuna
kashfa ya rushwa kwa waamuzi Ligi Kuu, kuna timu zinatuhumiwa kuhonga
marefa ili zisaidiwe kushinda, hili bado TFF haijatoka na jibu sahihi,
lakini kweli waamuzi wanavurunda. Pamoja na yote, matarajio yanabaki
pale pale, itakuwa ligi yenye ushindani mkubwa na ubingwa utapatikana
kwa jasho haswa.
Neema
zaidi imeletwa na kampuni ya Azam Media Limited iliyonunua haki za
matangazo ya Televisheni msimu uliopita, ambayo inafanya kila klabu
ipatiwe zaidi ya Sh. Milioni 100 kwa msimu. Wazi, fedha hizi zitasaidia
sana klabu, pamoja na zile za wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom maana yake
timu zitapunguza matatizo ya kifedha kwa kiasi kikubwa.
Mara
ya mwisho taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara lilitoka nje ya Dar
es Salaam mwaka 2000, walipolibeba Mtibwa Sugar ya Morogoro, lakini
tangu hapo timu tatu tu za Dar es Salaam zimepokezana taji, hilo Simba,
Yanga na Azam. Kuelekea msimu mpya, Simba, iliyotoka ndani ya tatu bora
imejiimarisha baada ya kupata viongozi wapya- Yanga na Azam bado wapo
vizuri. Mbeya City iliyomaliza nafasi ya tatu imejiimarisha pia, timu
zilizokuwa nje ya nne bora nazo zimejiimarisha. Zilizopanda nazo
kadhalika. Tarajia ligi moja tamu sana.
Karibu
Ligi Kuu, kilele cha ladha ya soka ya Tanzania. Zingatia, naitwa
Mahmoud Ramadhani Zubeiry, au BIN ZUBEIRY, ndiye nimeandika makala haya.
Furahia msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mabingwa; Azam FC wakiwa na taji lao baada ya kutwaa msimu uliopita. Je, wataweza kulitetea? |
EmoticonEmoticon