Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Kebwe Steven Kebwe (kulia)
akimkabidhi Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya
na Ustawi Dkt. Elias Chinamo moja ya kifaa (kamera) itakayotumika kupima
dalili za ugonjwa wa Ebola kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia
viwanja vya ndege ili kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama kwa
kuuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.
Mkurugenzi
wa Ugavi wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD),Heri Mchunga (kushoto)
akimpima Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na
Ustawi Dkt. Elias Chinamo (kulia) kuonyesha namna moja ya kifaa cha
kupimia joto la mwili wa Binadamu kinavyofanya kazi kwa kubaini dalili
za Ugonjwa wa Ebola eneo la uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es salaam.
Moja
ya kifaa (kamera) nne zilizoagizwa na Serikali kupimia dalili za
ugonjwa wa Ebola maeneo ya viwanja vya ndege. Kifaa hicho kina uwezo wa
kutunza picha na kumbukumbu za msafiri, muda , joto la msafiri, tarehe
aliyoingia nchini pia uwezo wa kupata takwimu kutoka kwenye hali ya
majimaji au jasho la Binadamu pindi kinapoelekezwa kwake.
Naibu
Waziri wa Afya Dkt. Kebwe Steven Kebwe akiongea na waandishi wa habari
eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa
kupokea na kukabidhi vifaa vya kupima dalili za ugonjwa wa Ebola.
Wengine ni Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Dharula na Maafa (kulia)
na Kaimu Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifani.
Naibu
Waziri wa Afya Dkt. Kebwe Steven Kebwe akiangalia kwa karibu taarifa
zilizorekodiwa na moja ya kifaa (kamera) nne zilizoagizwa na Serikali
kupimia dalili za ugonjwa wa Ebola maeneo ya viwanja vya ndege.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
………………………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Sehemu
ya vifaa vya kubaini hatua za awali za ugonjwa wa Ebola kwa kupima hali
ya joto la mwili kwa wasafiri kutoka nje nchi wanaotumia viwanja vya
ndege vilivyokuwa vimeagizwa na Serikali vimewasili jijini Dar es
salaam.
Vifaa
hivyo vinavyohusisha kamera 4 zenye uwezo wa kubaini joto la mwili wa
msafiri kwa umbali wa mita 100 bila kumgusa muhusika vimewasili leo
katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar
es salaam kutoka nchini Afrika ya Kusini vilikonunuliwa.
Akikabidhi
vifaa hivyo kwa wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Kebwe Steven Kebwe amesema kuwa
kuwasili kwa vifaa hivyo ni moja ya juhudi za Serikali za kuhakikisha
kuwa wananchi wanakuwa salama kwa kuuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.
Amesema
vifaa hivyo vitapelekwa katika maeneo ya viwanja vya ndege na maeneo
yanayotumiwa na raia wa kigeni kuingia nchini vikiwemo vya Dar es
salaam, Zanzibar, Kilimanjaro,Mbeya na Mwanza.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kuagiza vifaa zaidi vya kuwezesha
shughuli ya upimaji wa afya kwa wasafiri wanaotembea (scanners)
zitakazowezesha kubaini afya za wasafiri wengi zaidi kwa wakati mmoja
bila kulazimu kuwasimamisha.
Aidha,
amewataka wataalam hao wa afya kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa kwa
kuhakikisha wanawapima abiria wote wanaotoka nje ya nchi bila kujali
hadhi walizonazo ili kuweza kubaini kama wana maabukizi au dalili za
ugonjwa wa Ebola.
“Nataka
mfanye kazi yenu kwa kuzingatia weledi wa taaluma yenu na kwa
kuzingatia yale mliyojifunza,mvitumie vifaa hivyo kupima kila abiria ili
kubaini joto lake bila kujali cheo wala hadhi yake maana janga hili ni
kubwa” Amesema Dkt. Kebwe.
Kuhusu
utunzaji wa vifaa hivyo amewataka wataalam hao kuhakikisha wanavitunza
vifaa hivyo ili viweze kudumu na kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya
kuwasaidia wananchi kutokana na vifaa hivyo kugharimu fedha nyingi kila
kimoja.
Katika
hatua nyingine Mh. Kebwe amefafanua kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii inaendelea na shughuli ya utoaji wa Elimu ya Afya kuhusu ugonjwa
wa Ebaola ili kuwawezesha wananchi kuchukua tahadhari na kuzielewa
dalili za ugonjwa huo na namna ya kujingika endapo utagundulika nchini.
Amesema
tayari kamati mbalimbali za wataalam zimeshaundwa ili kuwezesha zoezi
la utoaji wa elimu na mafunzo kwa wataalam wa ndani ili kuwajengea uwezo
wa kukabiliana na janga hilo.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Cosmas
Mwaifwani ambaye ofisi yake imehusika katika uagizaji wa vifaa hivyo
nchini Afrika ya Kusini amesema kuwa mahitaji ya vifaa hivyo kwa sasa
yameongezeka kutokana na umuhimu wake na jinsi vinavyofanya kazi kwa
ufanisi mkubwa.
Amesema
upimaji kwa kutumia vifaa hivyo unatumia teknolojia ya kubaini mionzi
ya joto kutoka katika mwili wa binadamu pindi vinapoelekezwa katika
maeneo ya macho na masikio ya mwili wa binadamu.
Amefafanua
kuwa vifaa hivyo vinauwezo wa kutunza picha na kumbukumbu za msafiri,
muda , joto la msafiri na tarehe aliyoingia nchini na kuongeza kuwa
vifaa hivyo vina uwezo wa kupata takwimu kutoka kwenye hali ya majimaji
au jasho la Binadamu pindi kinapoelekezwa kwake.
Mwaifwani
ameeleza kuwa MSD inaendelea kuimarisha uwezo wake kwa kuongeza vifaa
zaidi kutoka Ubelgiji na China na kufafanua kuwa Bohari hiyo imejiandaa
kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa kujenga uwezo wa kuwa na dawa za
kutibu hali ya magonjwa yanayoambatana na homa hiyo.
Naye
Mkurugenzi wa Viwanja vya ndege nchini, Moses Malaki akizungumza kwa
niaba ya Viwanja vya ndege nchini ameielezea hali hiyo ya upatikanaji wa
vifaa katika maeneo hayo kuwa itaongeza ufanisi wa uchunguzi wa afya
kwa wasafiri na kuondoa usumbufu kutokana na uwezo wa vifaa hivyo
kumpima msafiri akiwa mbali.
EmoticonEmoticon