RAMBIRAMBI MSIBA WA MAKAMU WA RAIS FIFA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shrikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter kutokana na kifo cha makamu wake mwandamizi
Julio Grondora.
Amesema yeye binafsi na jamii ya mpira wa miguu
Tanzania kwa ujumla wanaomboleza msiba wa Grondora ambaye pia alikuwa Rais wa
Chama cha Mpira wa Miguu cha Argentina (AFA).
Ameongeza kuwa Grondora alikuwa mtumishi mwandamizi wa
mpira wa miguu, kwani alijitoa katika kuutumikia mpira wa miguu, na mchango
wake katika maendeleo ya mchezo huo utaendelea kukumbukwa wakati wote.
Rais
Malinzi amesema familia ya mpira wa miguu nchini Argentina imepata pigo, na ametoa
pole kwa familia ya marehemu, AFA na familia nzima ya FIFA na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana
ametoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina.
KLABU VPL, FDL ZATAKIWA KUWASILISHA MABENCHI YA UFUNDI
Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinatakiwa kuwasilisha Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) orodha ya watendaji wa mabenchi yao ya ufundi yakiongozwa
na Kocha Mkuu.
Ni wajibu wa klabu kuhakikisha
zinatekeleza maagizo hayo kwani ni matakwa ya Kanuni za VPL na zile za FDL.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara itaanza kutimua vumbi Septemba 20 mwaka huu wakati ile
ya FDL inatarajia kuanza Oktoba mwaka huu.
AZAM KUCHEZA MICHUANO YA KAGAME
Azam FC ndiyo itakayoiwakilisha
Tanzania Bara kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe
la Kagame) iliyopangwa kuanza Agosti 8 mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limeiteua Azam kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano hiyo
baada ya waandaaji wake, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na
Kati (CECAFA) kuamua kuindoa Yanga iliyokuwa icheze awali.
CECAFA imesema baada ya majadiliano
na Yanga kupitia TFF, klabu hiyo ilipewa muda hadi jana (Agosti 4 mwaka huu)
iwe imetekeleza matakwa ya kikanuni ili iruhusiwe kushiriki michuano hiyo
lakini haikufanya hivyo.
Yanga iliwasilisha orodha ya
wachezaji wengi wa kikosi cha pili kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo, jambo
ambalo limekatawaliwa na CECAFA kwa vile linakwenda kinyume na kanuni za
michuano hiyo.
Azam FC ambayo ilishika nafasi ya
pili- nyuma ya Yanga katika ligi iliyopita msimu wa 2012/2013 imekubali
kushiriki michuano hiyo na inatarajia kuondoka nchini kesho (Agosti 6 mwaka
huu) kwenda Kigali.
Msafara wa Azam FC katika michuano
hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, James Mhagama.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
EmoticonEmoticon