Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif
Rashidi akiwasha moja ya kati ya magari manne
aliyoyapokea kutoka kwa mwakilishi wa shirika la GLRA la Ujerumani nchini
Burchard Rwamtoga leo jijini Dar es salaam.
01. Mwakilishi
wa shirika la GLRA nchini Burchard Rwamtoga (kushoto) akimkabidhi Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi (kulia) ufunguo wa moja kati ya
pikipiki 20 zilizotolewa na shirika la hilo leo jijini Dar es salaam.
********************************
Eleuteri Mangi-MAELEZO
SERIKALI kupitia Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii imepokea msaada wa gari 4 na pikipiki 20 vyenye
thamani ya Tsh. Milioni 261 kutoka Shirika la GLRA kutoka nchini Ujerumani kwa
ajili ya kusaidia mapambano ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma nchini.
Mikoa ambayo imenufaika
na msaada huo ni pamoja na Tanga, Kigoma, na Mikoa ya Kanda Maalum ya Ilala na
Kinondoni.
Akipokea msaada huo leo
(Jumanne Agosti 26, 2014) Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi (Mb)
aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia kikamilifu matumizi ya
vyombo hivyo vya usafiri kwa kuvilinda na kuvitumia kulingana na malengo
yaliyokusudiwa.
Dkt. Seif alisema kuwa vifaa
hivyo vimegawiwa kulingana na mgawanyo wa mikoa iliyoanishwa na Serikali katika
Mpango wa Taifa wa kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma.
Dkt. Seif alisema Mpango
wa Taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma umekuwa na mafanikio ambapo imeendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa wote
wa kifua kikuu na ukoma bila malipo katika hospitali na vituo vya huduma za
afya vya serikali na binafsi nchini.
Aidha, Dkt. Seif
amesema kuwa Tanzania imevuka malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa
kuponyesha asilimia 85 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu wanaoanza matibabu kila
mwaka.
“Takwimu zinaonesha kuwa
Tanzania imefikia viwango vya asilimia 88 ya kuwahudumia na kuwaponyesha
wagonjwa hao ambayo ni zaidi ya kiwango cha WHO” alisema Dkt Seif.
Dkt. Seif amesema kuwa
kwa upande wa ugonjwa wa ukoma, Serikali inaendelea kufanya kampeni katika
mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Kagera, Lindi, Morogoro, Mwanza, Pwani, Rukwa,
Shinyanga, Tabora na Tanga katika kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga
na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Dkt. Seif
alisema wagonjwa wapya wa ukoma waliogunduliwa mpaka sasa na kupatiwa tiba ni
23,667, na Serikali tayari imetoa jozi 35,000 ya viatu maalumu kwa wagonjwa hao.
“Mpaka sasa tumeweza kufikia
malengo ya kimataifa ya kutokomeza ukoma kwa kuwa chini ya mgonjwa mmoja katika
watu 10,000 na kufanya ugonjwa wa ukoma kuwa si tatizo kubwa la kiafya kwa
jamii nchini” alisema Dkt Rashid.
Naye mwakilishi wa shirika
lisilo la kiserikali la GLRA nchini Burchard Rwamtoga aliusifu kwa ushirikiano uliodumu kwa miaka
37 baina ya Shirika hilo na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya magonjwa ya
ukoma na kifua kikuu.
Aidha, Rwamtoga
aliongeza kuwa Shirika la GLRA hutoa wastani wa Tsh. Bilioni 1.3 kila mwaka kwa
Serikali na kati ya fedha hizo kiasi cha
Tsh.milioni 600 hutumika kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya usafirishaji
ikiwemo magari, na pikipiki kwa waratibu wa kifua kikuu na ukoma.
GLRA mbali na kutoa
fedha kwa Serikali pia tunaratibu mpango wa
kuwajengea uwezo wa kiutendaji waratibu wa mikoa ikiwemo kutoa mafunzo
nje ya nchi kupitia kituo cha ALERT kilichopo nchini Ethiopia, ambacho
hujisihusha na mafunzo ya upasuaji na kutoa visaidizi ikiwamo miguu bandia na
baiskeli kwa wagonjwa.
Kwa upande wake Mratibu
wa huduma za kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ilala Dkt. Mbarouk Seif ameishukuru
Serikali kuupatia mkoa huowake gari la wagonjwa na kuahidi kuwa Ofisi yake
itahakikisha gari hilo linawafikia na kuwahudumia wagonjwa kwa wakati.
Shirika la GLRA ilianza kusaidia wagonjwa wa ukoma nchini mwaka 1959 na kupata usajili mwaka 1977 ambapo lilianza kushirikiana na Mpango wa Kudhibiti kifua kikuu na ukoma (NTLP) nchini uliopo chini ya Wizara ya Afya na Usatawi wa Jamii.
EmoticonEmoticon