STAILI
ile ile waliyotumia Yanga SC kumpata mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi ndiyo
ambayo klabu yake ya zamani, Simba SC inaitumia kumrejesha kundini Mganda huyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jioni hii mjini Dar es Salaam, Okwi amesema
kwamba amesaini Simba SC mkataba huru wa muda, baada ya Yanga SC kumpa barua ya
kusitisha mkataba naye jana pamoja na kumshitaki Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).
Okwi amesema ameamua kuomba kuichezea Simba SC kipindi hiki ambacho ana
matatizo na Yanga SC ili kulinda kipaji chake, kwa kuwa hata FIFA haitaki
mchezaji akae bila kucheza.
“Sasa wakati Yanga wanaendelea na kesi yao, mimi ninaomba nichezee
Simba SC ili kulinda kipaji changu. Nimewaandikia barua TFF na FIFA pia na nina
matumaini usajili wangu utaidhinishwa, kwa sababu mimi si tatizo katika
hili,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans
Poppe amesema kwamba wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala
lake na Yanga SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji.
“Baada ya kulipitia suala lake na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo
mchezaji mwenyewe ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze
mpira kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga
SC,”amesema Poppe.
Yanga mtanikoma; Okwi
akiwa ameshika jezi yake nbamba 25 kwa pamoja na Hans Poppe
Tayari Simba SC imetuma jina la mchezaji huyo katika usajili wake TFF
na ataungana na Mganda mwenzake, Joseph Owino, Warundi Pierre Kwizera na Amisi
Tambwe na Mkenya, Paul Kiongera katika wachezaji watano wa kigeni.
“Tumewaandikia barua TFF kuomba kumtumia mchezaji huyu kwa muda wakati kesi
yake na Yanga inaendelea, tumeambatanisha na barua yake ambayo yeye anatuomba
kucheza kwetu kulinda kipaji chake,”amesema Poppe.
Okwi aliichezea Simba SC tangu mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana
kuuzwa kwa dola za Kimarekani 300,000 Etoile du Sahel ya Tunisia. Etoile
haikulipa fedha hizo Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi,
aliyedai hakulipwa pia mishahara yake kwa miezi mitatu. Okwi akawafungulia
Etoile kesi FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea
timu yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao.
Akiwa SC Villa ndipo aliposaini Yanga SC Desemba mwaka jana na pamoja na
mapingamizi yaliyoanzia ndani, na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi
aliidhinishwa kuichezea timu hiyo ya Jangwani.
Okwi aliichezea Yanga
SC mechi 11 na kuifungia mabao matano- lakini kuelekea mechi tano za mwisho za
Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo. Okwi
alisusa kushinikiza amaliziwe fedha zake za usajili na mgogoro wao umeendelea
huku mchezaji huyo akiwa amesusa tangu Machi, miezi minne tu baadaye tangu
asajiliwe.
Vikao kadhaa
vimekwishafanyika baina ya Okwi na Yanga SC tangu hapo kutafuta suluhu ya suala
hilo na kikao cha mwisho leo baina ya mchezo huyo na Mwenyekiti wa klabu hiyo,
Yussuf Manji matokeo yake ni nyota huyo kurejea Msimbazi.
Kuhusu deni lao la
dola 300,000 kumuuza mchezaji huyo Etoile, Poppe amesema haihusiani kabisa na
usajili wake huu wa sasa. “Ile kesi yetu ya madai ya fedha zetu kule FIFA
ilikwishamalizika na vielelezo vyote vilipelekwa, bado kutolewa hukumu tu,”
amesema
EmoticonEmoticon