Na Anna Nkinda – Washington
Imeelezwa kwamba kutokuwa na uelewa wa kutosha
kuhusu ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, upungufu wa upatikanaji
wa huduma za afya, na vitendea kazi, utungaji wa sera zisizo rafiki,
pamoja na ukosefu wa takwimu za magonjwa ni moja ya sababu
zinazosababisha wanawake wengi kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete wakati akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wake wa
marais wa Afrika waliohudhuria hafla fupi ya chakula cha mchana
kilichoandaliwa na kituo cha Marais wa Afrika (African Presidential
Centre) cha chuo kikuu cha Boston iliyofanyika mjini Washington.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kwa kiasi kikubwa
kuna mahusiano kati ya ugonjwa wa Ukimwi na Saratani ya mlango wa kizazi
ambao kama mgonjwa atapata matibabu mapema atapona lakini kutokana na
uelewa mdogo baadhi ya wanawake wanapoteza maisha.
“Kutokana na utaalamu uliopo sasa
ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi unazuilika na kutibika lakini
bado kuna uelewa mdogo katika jamii kuhusu uhusiano uliopo kati ya
ugonjwa huu na ule wa Ukimwi; kama zitapatikana fedha za kutosha asasi
zisizo za kiserikali ambao ni wawezeshashi wataweza kutoa elimu kwa
jamii kuhusiana na magonjwa haya”, alisema Mama Kikwete.
Akiongelea kuhusu maambukizi ya
ugonjwa wa Ukimwi Mama Kikwete alisema ugonjwa huo unasababisha vifo vya
watu wengi lakini bado kuna magonjwa mengine ambayo ni tishio nchini
kama Malaria na Kifua kikuu ambayo nayo yanaua watu wengi.
Alisema, “Ugonjwa wa Ukimwi
unasababisha vifo vya wanawake wengi nchini kwa upande wa vijana watoto
wa kike wanaathirika zaidi ukilinganisha na watoto wa kiume na kwa watu
wazima wanawake wengi wanapata maambukizi zaidi ukilinganisha na
wanaume.
“Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi
yamepungua kutoka asilimia 7 kwa mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 5.1
mwaka 2012 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar
maambukizi ni asilimia 0.6% kwa miaka yote hiyo”
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema
vituo vya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) vimeongezeka kwa
sababu vituo vilivyokuwa vinatoa huduma ya uzazi na watoto wachanga hivi
sasa vinatoa huduma ya upimaji wa maambukizi ya VVU lakini bado
jitihada kubwa zaidi zinahitajika kufanyika ili kuwe na vituo vingi vya
kutoa huduma hiyo.
Kwa upande wa vifo vya watoto
wenye umri wa chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 147 kwa kila
vizazi hai 1000 kwa mwaka 1999 hadi kufikia vifo 81 kwa mwaka 2010. Vifo
vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 99 na
kufikia 51 kwa kila vizazi hai 1000 ingawa tatizo limepungua hatua zaidi
zinatakiwa kuchukuliwa ili kuimarisha afya ya watoto.
Kuhusu vifo vya kina mama
wajawazito alisema vimepungua kutoka 578 kati ya vizazi hai 100,000
mwaka 1996 hadi kufikia 454 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2010
hii inatokana na jamii kuwa na uelewa juu ya umuhimu wa mwanamke
kuhudhuria kliniki mapema pindi apatapo ujauzito na kujifungulia katika
vituo vya afya .
Mama Kikwete alisema, “Vifo vingi
vya kina mama wajawazito vinatokana na kutofuata uzazi wa mpango na
uchumi mdogo wa wanawake, utoaji wa mimba usio salama, kuvunja damu
nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba, kushindwa kujifungua,
uhaba wa huduma za haraka za uzazi na huduma za mtoto mchanga na uhaba
wa watoa huduma za afya waliobobea,”.
Aliendelea kusema vifo
vinavyotokea wakati wa kujifungua vinahusiana na afya ya mama wakati wa
ujauzito, hali ya kujifungua na jinsi ya kumjali mtoto wakati wa
kujifungua. Mwanamke atakayejifungua mtoto akiwa na umri mdogo atakuwa
na watoto wengi ambao umri wao haujapishana hayo yote yana madhara kwa
afya ya mama na mtoto .
“Ili kupunguza vifo vya kina mama
wajawazito na watoto wachanga, ugonjwa wa saratani ya matiti na mlango
wa kizazi na Ukimwi hasa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto Taasisi ya WAMA inafanya kazi ya uraghibishi kwa
kutoa vifaa tiba na elimu ya uzazi kwa vijana. Tunawakaribisha ili
tuweze kufanya kazi kwa pamoja ya kuokoa maisha ya mama na mtoto wa
Tanzania”, alisisitiza Mama Kikwete.
Akiwakaribisha wake hao wa Marais
Mkurugenzi wa Kituo cha Marais wa Afrika Balozi Charles Stith
aliwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya katika nchi zao ya kujali afya
ya mama na mtoto na kuwataka waendee na kazi hiyo bila ya kukata tamaa
kwani wao kama viongozi wanahitajika katika kutatua changamoto
mbalimbali zinazoikabili jamii inayowazunguka.
Balozi Stith alisema kituo chake kinatambua mchango wao na kazi wanayoifanya hasa katika kushughulikia afya ya mama na mtoto na upatikanaji wa elimu ya mtoto wa kike na kuhahidi kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana nao ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Balozi Stith alisema kituo chake kinatambua mchango wao na kazi wanayoifanya hasa katika kushughulikia afya ya mama na mtoto na upatikanaji wa elimu ya mtoto wa kike na kuhahidi kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana nao ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Mama Kikwete anauhudhuria mkutano
wa wake wa Marais wa Afrika ulioandaliwa na Mke wa Rais wa Marekani Mama
Michelle Obama kwa kushirikiana na Taasisi ya George W. Bush ambao
unajadili matatizo ya vifo vya kina mama wajawazito na watoto, ugonjwa
wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti na elimu ya mtoto wa kike.
EmoticonEmoticon