KATIBU wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga(UVCCM)Mwajuma Rashid ametoa wito kwa viongozi wa ngazi mbalimbali mkoani hapa waliochaguliwa na wananchi na kushindwa kutekeleza wajibu wao wasihangaike kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu 2015 kwani hawatawaunga mkono.
Mwajuma alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha kamati ya utekeleza ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama cha Mapinduzi uliopo mjini hapa .
Alisema katika kikao hicho waliweza kujadili mambo mbalimbali kubwa likiwemo suala la uchaguzi mkuu ujazo na kukubaliana kuwa vijana wenye uwezo wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi walijitokeze kwani wao watawaunga mkono kwa asilimia kubwa lengo likiwa kuleta mabadiliko na chachu ya maendeleo kwenye jamii.
Aidha alisema vijana wanapaswa kujithatiti na kuangalia namna ya
kuweza kuwania nafasi hizo kuanza ngazi za serikali za mitaa,udiwani na ubunge kwa malengo ya kuwapa maendeleo wananchi wanaowapa ridhaa ya kuwaongoza.
Alisema viongozi ambao walikuwa ni mizigo kwa kushindwa kuwajibika watambue kuwa jumuiya hiyo haitawaunga mkono hivyo ni bora waache kuchukua fomu na kusisitiza ikiwezekana watawafuata na kuwaeleza zaidi kuwa hawatoshi kugombea.
“Tupo mbioni kuwaambia ukweli wagombea ambao hawajatekeleza wajibu wao kwani hatupo tayari kukiona chama kinashindwa kupata ridhaa ya kuwaongoza wananchi kwa sababu ya kiongozi ambaye hatekelezi wajibu wake “Alisema Mwajuma.
Hata hivyo alizungumzia suala la makundi ambapo alisema hali hiyo
haiwezi kuzuilika ila wanapaswa kusubiri na kuwa na uvumilivu kwa sababu makundi ya tokea mwaka 2005 mpaka leo yapo lakini wanapaswa kuyavunja na kuanza upya kwa kuwaunga mkono wagombea waliojitokeza.
Mwajuma alisema kwa sababu kuzuia makundi kwenye chama ni kazi ngumu lakini wakishapatikana wagombea kuyavunje na kueleza makundi hayo zaidi yanakuwa na wapambe na kuwataka wapambe kuwa wagombea wao wanaposhindwa basi wakubaliane na matokeo.
EmoticonEmoticon