April 02, 2014

Salaam. Kocha Mkuu wa Simba,  Zdavko Logarusic ‘Loga’  ametimiza mechi 10 za Ligi Kuu Bara akiwa amekusanya pointi 12  lakini amezidiwa na Abdalah Kibadeni, ambaye aliinoa na timu  hiyo kwenye mzunguko wa kwanza kwani alikusanya pointi 20 katika idadi hiyo ya mechi.
Simba ikiwa chini ya Loga tayari imepoteza nafasi ya kuwania nafasi tatu za juu baada ya kufungwa Jumapili iliyopita na Azam 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo kubaki nafasi ya nne na pointi zake 36.
Azam inaongoza ligi ikiwa na pointi 53, wakifuatiwa na Yanga (46) na Mbeya City imekamata nafasi ya tatu na pointi 45 wakiiacha Simba kwa tofauti ya pointi tisa wakati zimebakiza michezo mitatu.
Loga alikabidhiwa jukumu la kuinoa Simba, Desemba mwaka jana baada ya uongozi wa klabu hiyo kumfuta kazi Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo kwa madai ya kutoridhishwa na matokeo ya timu yao.

Wakati huo Simba ilikuwa ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24.

Kibadeni alidumu katika klabu hiyo kwa kipindi kisichozidi miezi sita na kuiongoza kushinda mechi tano, wakitoka sare tano katika michezo 10 kabla ya kufungwa na Azam.

Mcroatia huyo aliyeanza kibarua chake kwa kishindo kwa kuiongoza Simba kushinda mabao 3-1 dhidi ya Yanga katika mechi ya kirafiki ya `Nani Mtani Jembe’, alishindwa kuhamisha mafanikio hayo katika ligi.

Tangu Januari 26, mwaka hu, Loga ameiongoza Simba kushinda mechi tatu tu, akitoka sare tatu pamoja na kufungwa mechi nne dhidi ya Mgambo Shooting (1-0),  Coastal Union SC (1-0), JKT Ruvu (2 - 3) na Azam FC 2-1.

 Logarusic alisema: “Nashangaa tunacheza sisi lakini tunafungwa, nafikiri ni kutokuwa makini, tunacheza kwa kufikiria pasi na mashuti,” alilalamika kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya.

Naye nahodha wa Simba, Nassor Masoud ‘Cholo’ alisema matokeo mabaya waliyoyapata kwenye kipindi hiki ni funzo kwao na sasa wajipange kwa ajili ya msimu ujao.

Cholo alisema: “Tulichokipata, kinatukumbusha kuwa, duniani kuna kupanda na kushuka, sisi tumeshateleza haina jinsi, tukubaliane tu na matokeo haya.”

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »