April 07, 2014

KINANA, NAPE KUTUA KIGOMA KESHO ASUBUHI


NA BASHIR NKOROMO, KIGOMA
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, anatarajiwa kutua Kigoma kesho, kuanza ziara ya siku tano mkoani hapa.
Ratiba iliyotolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Kigoma, Mohamed Nyawenga, inaonyesha kuwa mapokezi ya Kinana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kigoma, uliopo eneo la Kipampa, Ujiji yatafanyika kuanzia saa 3.00 asubuhi na kumalizika saa 4.00 asubuhi.
Kulingana na ratiba hiyo, baada ya kutoka Uwanja wa Ndege, Kinana ataenda Ofisi ya CCM mkoa wa Kigoma, ambako atafanya shughuli kadhaa ikiwemo kusaini kitabu cha wageni na kupokea taarifa ya Chama, kuzungumza na Kamati ya Siasa ya mkoa na baadaye kufungua mradi wa maduka.
Baada ya kupumzika  kati ya saa 6. 00 hadi saa 7. 00 mchana, Kinana ataondoka na msafara wake kwa njia ya boti kupitia ziwa Tanganyika, kwenda Hifadhi ya Taifa ya Gombe ambako atatembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kufahamu changamoto na mafanikio zilizopo kwenye rasilimali hiyo ya nchi.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa, Aprili 9, 2014, Kinana atakwenda wilaya ya Kasulu ambako baada ya kusaini kitabu wilayani na kuzungumza na katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya wilaya hiyo, atafanya shughuli kadhaa katika Kata mbalimbali.


Kinana anaaza ziara hiyo, baada ya juzi kumaliza nyingine ya siku sita katika mkoa wa Rukwa, ambako katika ziara hiyo alikagua uhai wa chama, utekelezaji wa ilani na Chama na kusikiliza kero za wananchi huku akijadiliana nao njia za kuzitatua pale zilizpojitokeza.
Wakati huohuo, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye pia anatarajiwa kutua mkoani Kigoma, kesho asubuhi, kuungana na Kinana kwenye ziara hiyo.

Nape anaungana na Kinana baada ya kumaliza shughuli pevu ya kuratibu kampeni za CCM za uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze. Kampeni hizo zilimalizika juzi na uchaguzi wake kufanyika jana ambapo CCM imeibuka kidedea kwa kuzoa kura nyingi.

Kutokana na theNkoromo Blog kupata fursa ya kuwepo Kigoma, itakuwa ikijitahidi kuwahabarisha hasa kwa picha matukio yatakayoambana na ziara hiyo ya Kinana.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »