Balozi
Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang
akiwasilisha agizo la Serikali yake kwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi la kuridhia na kukubali kusaidia Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung uliopo Mtaa wa Mpirani - Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Balozi
Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Xie Yunliang akibadilishana mawazo na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake
ndani ya Jengo la Pius Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.Pembeni yao upande wa kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibarf Mh. Mohamed Aboud Mohamed.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiishukuru Serikali
ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Balozi Wake Mdogo aliyepo Zanziobar
Bw. Xie Yunliang kwa kukubali wazo la SMZ la kuiomba China kusaidia
ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung Jina linalotokana na Muasisi
wa Taifa hilo la China.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR)
Na Othman Khamis OMPR.
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China
imeridhia na kukubali kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha michezo
kilichopewa jina na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Mau Tse Tung
kilichopo miperani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa
Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yunliang wakati
akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
hapo katika Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Msekwa Bungeni Mjini
Dodoma.
Balozi Xie Junliang alimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Timu ya wataalamu wa China inatarajiwa
kukifanyia utafiti na uchunguzi kiwanja hicho baadaye mwaka huu sambamba
na utiwaji saini Makubaliano ya ujenzi wa kiwanja hicho unaotarajiwa
kufanyika mapema mwaka ujao.
Alisema ujenzi wa uwanja huo uliopewa
heshima ya Jina la Kiongozi muasisi wa Taifa la China Marehemu Mao Tse
Tung utajumuisha kiwanja cha mchezo wa soka pamoja na michezo mengine ya
ndani mfano mchezo wa Table Tennis.
“ Tunatarajia ujeni wa kiwanja cha Mao
utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanamichezo wa michezo
tofauti ukiwemo ule unaopendwa zaidi wa soka “. Alisema Bwana Xie
Junliang.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar
alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano wa kidugu
uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na China
unastahiki kuenziwa zaidi.
Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba
Jamuhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla katika harakati zake za kujikwamua kiuchumi.
Alisema matengenezo makubwa ya ujenzi wa
Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Kisiwani Pemba, ujenzi wa
maegesho ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar pamoja
na matayarisho wa matengenezo ya chumba cha wagonjwa mahututi { ICU }
mwezi Juni mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ni miongoni mwa
uthibitisho wa uhusiano wa pande hizo mbili.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jamuhuri ya Watu wa
China kwa moyo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla katika miradi ya Kiuchumi na Maendeleo.
Balozi Seif alisema mchango wa Serikali
ya China kwa Zanzibar umesaidia kuiwawezesha asilimia kubwa ya Jamii
Zanzibar kustawika Kijamii na hata kiuchumi kupitia miundo mbinu
iliyowekwa na Serikali kwa msaada wa Nchi hiyo rafiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alitolea mfano msaada mkubwa uliotolewa na China katika ujenzi wa skuli
za Wilaya za Sekondari katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Alisema mradi huo mkubwa wa sekta ya
Elimu umekuja kufuatia ongezeko kubwa la idadi wa wanafunzi
wanaofanikiwa kujiunga na masomo ya Sekondari katika maeneo tofauti ya
Zanzibar.
“ Kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi
hasa eneo la Wilaya ya Magharibi katika Kisiwa cha Unguja
tumelishuhudia hivi karibuni katika skuli ya Kijitoupele na Serikali
kupitia Wizara ya Elimu tunaliangalia tatizo hilo kwa mtazamo wa kujenga
skuli mpya katika Mtaa wa Pangawe “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliipongeza China kupitia Balozi wake huyo kwa mchango wake mkubwa
katika Nyanja ya Elimu mchango ambao tayari watoto wa Zanzibar
wanaendelea kufaidika nao.



EmoticonEmoticon