YANGA YALITIKISA JIJI LA TANGA,COASTAL KUWAFUNGA MIDOMO YANGA KESHO.

January 28, 2014


  Kocha wa Yanga,Hans Van Der Pluijm kulia akitoka kwenye uwanja wa Mkwakwani leo asubuhi mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo kushoto ni Ofisa Habari wa timu hiyo,Baraka Kizuguto.
TIMU ya Dar es Saalam Yanga Africa imetua jijini Tanga juzi na kulakiwa na wapenzi pamoja na wanachama wao wakiwa na matumaini makubwa kuweza kuibuka na ushindi kwenye mechi yao dhidi ya Coastal Union ya Tanga kesho 

Mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kwenye dimba la CCM Mkwakwani unatarajiwa kuwa mkali na upinzani wa hali ya juu kutokana na timu zote kufanya maandalizi nje ya nchi kwa Yanga kwenda Uturuki na Coastal Union wao wakitokea Omani.

Yanga wao waliwasili mkoani Tanga juzi wakitokea jijini Dar es Salaam wakiwa wachezaji wao 20 ambao watatumika kwenye mechi hiyo na kufanya mazoezi kwenye viwanja vya Gymkana na CCM Mkwakwani wakiwa na idadi kubwa ya mashabiki waliojitokeza kuwaona wachezaji mahiri wa timu hiyo.

Mazoezi ya timu hiyo yalikuwa yakiongozwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mholanzi Hans Van Der Pluijm akisaidiana na Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali “Mensa”ambayo yalikuwa wakianza saa moja asubuhi mpaka saa tatu asubuhi.

Akizungumzia mechi yao na Coastal Union ya Tanga, Hans Van Der Pluijm alisema alichofuata mkoani hapa ni kuhakikisha anachukua pointi tatu na sio kitu kingine kwani wachezaji wake wana kiwango kizuri ambacho kinafanikisha malengo yake hayo.

Kocha huyo alisema msimu huu matarajio yake makubwa ni kutaka kuendelea kuchukua ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara akisema hilo linawezekana kutokana na uongozi imara na mshikamano uliopo kwenye klabu hiyo.

Hata hivyo Kocha huyo aliwataka wachezaji wake kutumia akili wanapokuwa mchezoni pamoja na kucheza pasi ndefu kwani hiyo ndio silaha ya ushindi kwenye mechi zao kwenye mzunguko huo wa pili wa ligi kuu hapa nchini.


         “Mnapaswa kubadilika na kucheza pasi ndefu ndefu pamoja na kutumia akili pindi muwapo mchezoni kwani aina hivyo inaweza kutupa mafanakio makubwa sana siku za mbele kwenye michuano hii “Alisema Mholanzi Van Der Pluijm.

Wakati Yanga wakiwa Uwanja wa CCM Mkwakwani wapinzani wao Wagosi wa Kaya “Coastal Union” wao wanafanya mazoezi kwenye dimba la soka Gymkan wakiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo

Msemaji wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Hafidhi Kido aliliambia gazeti hili kuwa mechi hiyo haitakuwa rahisi sana kama watu wengi wanavofikiria kwa sababu wao wamedhamiria kuhakikisha wanapata pointi tatu na hilo litawezekana kutokana na kuimarika kikosi hicho.

  “Mechi hii ni ngumu hivyo tutahakikisha tunashinda ili tuwafunge midomo Yanga na hili ndilo ambalo litadhihirisha kuwa hatukwenda Omani kutalii bali kuweka kambi “Alisema Kido.

Aidha kwa upande mwengine, Mashabiki wa Coastal Union wameitabiria timu yao ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga kwenye mechi hiyo wakisema wanaamini kikosi kimekamilika kwa asilimia.

Hali ya Jiji la Tanga imeonekana kubadilika kwa pilika pilika kuelekea mchezo huo huku baadhi ya mashabiki na wapenzi wakiwa kwenye maeneo mbalimbali wakinunua tisheti za timu hizo mbili wakati wengine wakinunua zile za Simba.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »