Na Hadija Bagasha Muheza,
MAABARA ya kupima ubora wa maji Mkoani Tanga imesema kuwa visima tisa
vya maji vilivyochimbwa katika mji mdogo wa Muheza maji yake yameonekana kuwa na ubora mzuri na kubainika kuwa yanafaa kwa matumizi ya binadamu.
Taarifa hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja wa Maabara ya Maji mkoa wa Tanga Rukia Tuwano na kupewa nakala Mbunge wa jimbo la Muheza Herbert Mntangi.
Alisema kuwa kazi hiyo ya vipimo vya maji imegharimu shilingi 1848000 na kueleza kuwa uchunguzi wa ubora wa maji umefanyika na kilichogundulika ni kwamba maji kutoka katika vyanzo vyote vya visima tisa yanafaa kwamatumizi ya nyumbani.
Tuwano alisema kuwa visima viwili ambavyo ni cha Michungwani Tank na Michungani kwa Mafua vimeonekana ni safi kwa kutokuwa na Bacteria huku visima saba vimeonekana kuchafuliwa na Coliform bacteria na kusema kuwa visima hivyo vinatakiwa kuwekwa dawa ya kuulia Bacteria hao.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Muheza Herbert Mntangi alisema kuwa visima hivyo tisa vinne vipo maeneo ya Genge na vitano vipo maeneo ya Lusanga.
Mntangi alisema kuwa kwa taarifa hiyo sasa kamati ya madiwani ya
Elimu,Afya na Maji baada ya kupokea taarifa hiyo toka kwake Mbunge imeagiza ununuzi wa Pampu kwa visima vya Michungwani Tank na Michungwani kwa Mafua ili wananchi waweze kufaidika na huduma hiyo.
Mbunge huyo aliagiza ununuzi huo ufanyike haraka ili huduma hiyo ya maji iweze kupatika na wilayani hapo kwa lengo la kupunguza changamoto kubwa ya majini inayowakabili wakazi wa Muheza.
Mntangi aliwahakikishia wajumbe wa kamati hiyo katika kikao
kilichofanyika juzi ukumbi wa Bomani wilayani Muheza kwamba
zitapatikana fedha shilingi 273’000 000 wiki hii na kazi itaanza mara moja huku wakisubiri ahadi ya shilingi Bilioni 1 iliyotolewa na Waziri wa maji Jumanne Maghembe ambayo itasaidia kusambaza miundo mbinu ya maji Muheza mjini.
Alisema kuwa visima hivyo viwili vinatoa maji mengi lita Laki nne kwa siku moja ambapo visima vyote tisa vikikamilika kuwekwa pampu vitatoa Lita Milioni 1.6 kwa siku ambapo shida ya maji itapungua mji wa Muheza wakisubiri mradi mkubwa wa mto Zigi ambayo ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete.
Mntangi alisema kuwa kata ambazo zitafaidika na mradi huo wa visima tisa ni Majengo’ Genge,Mbaramo, Tanganyika,Masuguru’ Lusanga,Kwamkabarana Michungani na kwamba endapo fedha zitapatikana shida ya maji Muheza mjini itakuwa imeisha.
Mtangi alikemea tabia ya kuchezea fedha za miradi kama hiyo zinapokuja halmashauri kama zamani zaidiya shilingi Milioni 150 wamenunua mabomba na koki mbovu huku fedha zilizobakia wamekula ambapo Mwenyekiti wa halmashauri ya Muheza Amiri Kiroboto alithibitisha hilo.
Alisema kuwa kwa upande wa miradi ya maji vijijini tayari wametekeleza mradi wa Ubembe maji yanatoka na watayafikisha vijiji vya Misongeni mpaka Mikwamba yataungana na mradi mkubwa wa Magoroto yatakwenda mpaka Muheza mjini.
EmoticonEmoticon