RAIS MALINZI MGENI RASMI TUZO ZA MAKOCHA BORA MACHI 8 DAR ES SALAAM.

January 23, 2014
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.
RAIS wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya tuzo ya makocha wa mpira wa miguu Tanzania inayotarajia kufanyika Machi 8, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mtandao huu jijini Dar, Afisa Mtendaji wa tuzo hiyo, Fredrick Luunga alisema kamati ya maandalizi ya tuzo iliyokutana hivi karibuni ndiyo iliyopitisha jina la Malinzi kuwa mgeni rasmi siku hiyo.

Luunga alisema lengo la kumwalika kiongozi huyo wa juu wa soka ni kuthamini mchango wake katika kuendeleza mchezo huo hapa nchini na pia kumpa fursa ya kukutana na kuzungumza na makocha wa mpira wa miguu Tanzania na wadau wengine kupitia hafla hiyo.

Kuhusu maandalizi ya tuzo hiyo kiujumla, afisa huyo alisema yanakwenda vizuri na kwamba wapo katika mchakato wa kutafuta wadhamini zaidi.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na kamati imekuwa ikikutana mara kwa mara kwa lengo la kupanga mikakati mbalimbali”, alisema.

Hata hivyo, Luunga ametoa wito kwa wafadhili wa michezo nchini kujitokeza na kudhamini tuzo hiyo itakayokuwa ikitolewa kila mwaka.

“Bado tunahitaji wafadhili zaidi ili kufanikisha utoaji wa tuzo hizo kwani lengo ni kuhakikisha makocha wa soka nchini wanathaminiwa kutokana na kazi zao wanazofanya katika taaluma ya ukocha”, alisema.

Wakati huo huo, afisa huyo alisema zoezi la kuwapigia kura makocha wanaostahili kupata tuzo hizo linaendelea kwa kuandika katika simu neno sokafasta acha nafasi kisha jina la kocha yeyote na tuzo anayostahili kupata kisha itumwe kwenda 15678.

Tuzo zinazotarajiwa kutolewa siku hiyo ni kocha bora wa mwaka 2013, kocha bora wa makipa, kocha bora mkongwe mwenye mafanikio makubwa, kocha bora chipukizi, kocha bora wa kike, kocha bora wa kigeni, kocha bora wa kigeni aliyewahi kupata mafanikio makubwa nchini na kocha bora Mtanzania anayefundisha soka nje ya nchi kwa sasa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »