ZIUNGENI MKONO TAASISI ZINAZOPAMBANA NA UKATILI NA UNYANYASAJI WA WANAWAKE NA WATOTO-TUNU PINDA.

December 05, 2013
Na Paskal Mbunga,Tanga.
 MKOA wa Tanga umehimizwa kuziunga mkono taasisi zinazopambana dhidi ya ukatili na unyanyasi kwa wanawake na watoto ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa.

Akizindua rasmi leo kampeni ya “Tunaweza Mkoa wa Tanga” inayoerndeshwa na asasi ya Tree of Hope ya jijini hapa, Mke wa Waziri Mkuu Tunu Pinda alisema suala la ukatili wa kijinsia katika jamii yetu linaendelea kushika kasi na kuleta madhara mengi yakiwemo ulemavu mwilini, msongo wa mawazo, kuvunjia kwa ndoa ama kusababisha wanandoa kuathiriwa na magonjwa hatari, ukiwemo UKIMWI, na wakati mwingine vifo.


Mama Pinda alisema kwamba Mkoa wa Tanga umefikisha asilia 15.7 kwa ukatili wa kimwili (physical violence) na asilimia 11.3 ya matukio ya ukatili wa kingono (sexual violence).  Hii ni kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa mwaka 2010 (Tanzania Demographic & Health Survey),

Mke wa Waziri Mkuu ambaye alionekana kutishwa na takwimu hizo, aliutaka uongozi wa Mkoa wa Tanga kuchukua hatua za makusudi za kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa huku akionya kwamba hali hiyo sio ya kufumbiwa macho.

Alisema ili kupambana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania ilitunga sera ya Jinsia ya mwaka 2000 ikiandaa Mkakati wa miaka 15 wa kuondoa ukatili kwa wanawake na watoto katika jitihada ya kukabiiliana na changamoto hizo.

Mama Pinda alikemea tabia potofu zilizozoeleka miongoni mwa wanawake kwamba kupigwa na mume ni jambo la kawaida na linalokubalika kwa baadhi ya makosa ambayo mwanamke anapomkosea mumewe ni lazima aadhibiwe.

Alitaja mazoea hayo ni pamoja na kuafiki kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe iwapo ataondoka bila kuaga kwa mume. Pia mume ana haki ya kumpiga mkewe endapo atazembea kuangalia watoto.  Pia tabia nyingine ni mke kukubali kupigwa na mume kutokana na kubishana naye.

Mama Pinda alizitaka asasi za kiraia kuungana pamoja katika mapambano dhidi ya ukatili wa kinsia na kusisitiza kwamba kampeni ya “Tunaweza”Ni mkakati muhimu katika kutokemeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi katika ufunguzi huo uliofanyika katika uwanja wa Mkwakwani, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa aliwataka wakinamama kuiunga mkono kampeni hiyo kwa kujishughulisha na miradi ya uzalishaji mali ambayo kwayo itawaweka huru pasi na utegemezi mkubwa kutoka kwa wanaume. 
Aliwataka akinamama kuzitumia taasisi ya kifedha kwa ajili ya kujijengea mitaji ya kufanya biashara.
Kwa upande wake,Mratibu wa Asasi ya Tree of Hope FortunataManyeresa aliitaka jamii kuwa mstari kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwemo kuwalinda watoto na wanawake.
 Alisema asasi hiyo tayari imeshaeneza huduma zake katika wilaya zote nane za mkoa wa Tanga lengo likiwa ni kuhamasisha wakazi wa mkoa wa Tanga kupata mwamko wa kuweza kupambana na tatizo hilo ambalo lilojengeka kwa misingi ya tamaduni za kikabili.
  

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »