TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA TFF LEO

December 06, 2013
Release No. 206
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 6, 2013

TUMEJIANDAA VIZURI KWA MECHI- TANZANITE
Tanzanite imesema iko vizuri kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) inayochezwa kesho Jumamosi (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Tanzanite, Rogasian Kaijage amesema wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni.


“Tumejiandaa, vijana wako vizuri wanasubiri saa ya mechi tu. Licha ya kwamba Afrika Kusini wako mbele kwenye mpira wa miguu wa wanawake si sababu ya matokeo,” amesema Kaijage.

Amesema anaamini vijana wake watafanya vizuri, na kuwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kuwashangilia ili waweze kupata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.

Naye nahodha wa Tanzanite, Fatuma Issa amewataka Watanzania kuwaamini kwani wamejipanga kwa ajili ya pambano hilo, hivyo wawe nyuma yao katika kuwaongezea ari ili waweze kufanya vizuri.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na orange, sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A watalipa sh. 10,000. Tiketi zitauzwa uwanjani katika magari maalumu.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

RAMBIRAMBI MSIBA WA NELSON MANDELA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela kilichotokea jana (Desemba 5 mwaka huu) nchini humo.

Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwa Afrika Kusini, Afrika na Dunia kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa wa Mzee Mandela katika mchezo huo.

Mzee Mandela anakumbukwa kwa mchango wake katika Fainali za Afrika (AFCON) zilizofanyika mwaka 1996 nchini Afrika Kusini na hata zile za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini humo mwaka 2010.

TFF tunatoa pole kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA), Danny Jordan, na wananchi wa Afrika Kusini na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Mandela mahali pema peponi. Amina.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »